Queen Said ni mratibu wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio nchini Tanzania. Katika mahojiano
maalum na Radio Vatican kuhusu tatizo la vijana kutoka nchi zilizoendelea na kwa namna
ya pekee kutoka Barani Afrika kupenda kuzamia Ulaya na Marekani wakitafuta malisho
ya kijani kibichi anasema, kila mtu anayo haki ya kubaki na kuishi katika nchi yake
mwenyewe. Kwa njia hii vijana wanaweza kutumia fursa na rasilimali iliyopo nchini
mwao kujiendeleza wenyewe, kwa ajili ya familia na nchi zao katika ujumla wake.
Queen Said
ambaye bodo ni kijana kabisa aliyehitimu masomo yake hivi karibuni na kwa sasa anafanya
kazi kwenye Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Moshi, Mkoani Kilimanjaro, Tanzania anapenda
kuwashauri vijana wenzake wenye mawazo ya kuzamia ughaibuni wakidhani kwamba, wataweza
kupata maisha bora zaidi, kuachana na ndoto kama hizi, kwani wengi wao wanapofika
Ulaya na Marekani wanakumbana na adha, madhulumu, nyanyaso na kwa sehemu kubwa kifo,
kama inavyojitokeza sehemu mbali mbali za dunia.
Vijana hao mara nyingi wanajikuta
wakiangukia kwenye mikono ya wafanyabiashara haramu ya binadamu. Wakiwa nchini mwao,
wana uwezo na fursa nyingi za kuweza kukabiliana na changamoto za maisha, kumbe, ushauri
mkuu ni kwa vijana kubaki nchini mwao ili waweze kujiendeleza. Maisha Ulaya na Marekani
ni tofauti kabisa na vile yanavyooneshwa kwenye Luninga na vyombo mbali mbali vya
mawasiliano ya Jamii. Anasema, "usiwaone Wamasai wamevaa lubega rangi nyekundu ukadhani
wote ni washabiki wa Timu ya Simba"! Huo ni utamaduni na mavazi yao!
Queen
Said anasema, kuna sababu nyingi zinazopelekea watu kuzikimbia nchi zao: maafa asilia,
vita, kinzani, hali mbaya ya uchumi, madhulumu na nyanyaso mbali mbali, yote haya
ni mambo yanayopaswa kuangaliwa kwa jicho la mshikamano unaoongozwa na kanuni ya auni.
Serikali za nchi mbali mbali zitambua na kuthamini utu na heshima ya kila
mkimbizi anayeomba hifadhi ya maisha yake, kwa kuzingatia sheria, kanuni na mikataba
ya kimataifa. Ikumbukwe kwamba, hata wakimbizi katika shida na mahangaiko yao, wameumbwa
kwa sura na mfano wa Mungu, wana utu na heshima yao kama binadamu!