2013-07-08 07:53:10

Waseminari na Wanovisi wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuendelea kuwa waaminifu kwa Kristo, Kanisa na Watu wa nyakati hizi!


Maadhimisho ya Siku ya Majandokasisi na Wanovisi kutoka sehemu mbali mbali za dunia, limekuwa ni tukio ambalo limetoa fursa kwa vijana hawa ambao wako katika hija ya majiundo yao kama Mapadre na Watawa, kupata Katekesi ya kina kuhusu maisha na wito wa Kipadre na Kitawa ndani ya Kanisa Katoliki.

Wamebahatika kusikiliza ushuhuda uliotolewa na watu mbali mbali ambao wameonja furaha, karaha na magumu ya maisha ya Kipadre na Kitawa, lakini wakapiga moyo konde na kusonga mbele kwa imani na matumaini. Wameangalia Filamu ya Padre aliyepoteza maisha yake akiwa anahamasisha miito huko Kaskazini mwa Italia.

Askofu mkuu Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya, akimwalika Baba Mtakatifu Francisko kuzungumza na Majandokasisi pamoja na Wanovisi, amegusia kuhusu Waraka wa Kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko, Mwanga wa Imani, unaowakumbusha waamini kwamba, kwa mtu anayeamini, anaweza kuona. Anamshukuru Baba Mtakatifu kwa zawadi hii kubwa kwa Kanisa wakati huu wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Hii ni changamoto ya kuendelea kuwa ni waaminifu kwa Kristo, Kanisa na watu wa nyakati hizi.

Majandokasisi na Wanovisi wakati wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, kila mtu kwa lugha yake mwenyewe, aliweza kukiri kwa mara nyingine tena Kanuni ya Imani. Lugha zilikuwa ni nyingi, lakini zote ziliunganika katika Imani moja. Hawa ni vijana kutoka katika nchi 66, ambao wamewawakilisha vijana wenzao ambao wanaendelea kufanya hija ya maisha na wito wa kipadre na kitawa, wakipania kujitosa kimaso maso kwa ajili ya kumtumikia Mungu na jirani.

Ni jambo la haki na busara kwamba, katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Majandokasisi na Wanaovisi wapate siku yao maalum kwa ajili ya kuadhimisha Mwaka wa Imani. Hii ni fursa pia ya kujiandaa kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani huko Rio de Janeiro. Viajana hawa wamesali kwenye kaburi la Mtakatifu Petro, wamekutana na vijana wenzao kutoka sehemu mbali mbali za dunia; wameshirikishana furaha, wasi wasi na mang’amuzi juu ya maisha na wito wao.

Askofu mkuu Fisichella anasema kwamba, imani inahitaji kuona, kusikia na kugusa! Haya ndiyo mang’amuzi waliyopata vijana wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Waseminari na Wanavisi katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Hii ni hatua makini katika mchakato wa majiundo yao kama watawa, mapadre na wamissionari, tayari kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Uinjilishaji mpya, wakiwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, kwani wameutafakari uso wa Kristo kwa imani mkubwa!








All the contents on this site are copyrighted ©.