Katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo, Kanisa linapaswa kujikita zaidi
na zaidi katika maisha ya utume wa kimissionari, tayari kwenda sehemu mbali mbali
za dunia kutangaza Habari Njema ya Wokovu, daima likiendelea kutembea katika njia
ya uaminifu mintarafu maagizo ya Kristo mwenyewe. Ni changamoto na mwaliko kwa vijana
kushiriki kikamilifu katika maisha ya kitawa na kimissionari.
Ni maneno ya
Baba Mtakatifu Francisko kwa umati mkubwa wa Majandokasisi, wanovisi na vijana ambao
wako kwenye majiundo ya maisha na utume wa Kipadre na Kitawa, waliokuwa wamekusanyika
mjini Vatican kwa ajili ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Tafakari ya Baba Mtakatifu
ili sheheni majadiliano ya kina kati ya vijana, kwa kuwataka kuwa makini na malimwengu
yanayoweza kuwapotosha katika safari ya maisha yao ya kiroho na kiutu.
Wajipange
barabara na kamwe wasifanye mambo kwa kubahatisha kwani hali kama hii ina hatari kubwa
katika maisha na ustawi wa vijana. Vijana wajipange na hatimaye, wachague wito wanaotaka
kufuata katika maisha yao, ikiwa ni maisha ya ndoa na familia, basi wahakikishe kwamba,
wanakuwa ni wazazi bora na mafano wa kuigwa na jirani zao. Ikiwa kama watachagua kuwa
ni Mapadre na Watawa, basi wajitose kimaso maso bila ya kujiachilia kwa ajili ya Mungu
na jirani.
Vijana wajisikie kuwa na furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo
mwenyewe na wala si kwa vile wanamiliki simu nzuri ya kiganjani, Pikipiki ambayo ikipita
mtaani kila mtu "anakata shingo" au kwa kuwa na gari la kifahari. Yote haya ni mambo
ya mpito anasema Baba Mtakatifu Francisko na kamwe hayawezi kumpatia kijana furaha
ya kweli katika maisha!
Anasema, anasikitishwa kuona jinsi ambavyo Mapadre
na Watawa wanavyokimbilia kuwa na magari ya fahari. Anatambua umuhimu wa gari kwa
ajili ys shughuli za kichungaji, lakini kuna haja ya kuwa na busara na kiasi katika
manunuzi na matumizi ya vyombo vya usafiri, kwa kutambua kwamba, kuna watu wanaoteseka
sehemu mbali mbali za dunia, watu ambao wanahitaji kuonja: upendo, huruma na ukarimu
kutoka ndani ya Kanisa.
Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana kwamba, wao ni
muhimu na watu wa maana sana mbele ya Mwenyezi Mungu, ndiyo maana amewachagua ili
waweze kushiriki katika utume wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia,
kama Mapadre, watawa na Wamissionari. Wao wanapaswa kutoa jibu makini, linaoonesha
upendo wao kwa Mwenyezi Mungu.
Hii ndiyo siri ya furaha ya vijana wanaojitosa
kimaso maso kwa ajili ya Mungu na jirani. Ni mwaliko wa kuchuchumilia utakatifu wa
maisha kwa kuishi kwa uaminifu mashauri ya Kiinjili; yaani: Utii, Ufukara na Useja,
mambo yanayoonesha ubaba na umama katika utekelezaji wa mikakati ya shughuli za kichungaji.
Waseminari na Watawa watambue kwamba, upendo wao kwa Yesu ni wa hali ya juu kabisa
kwani unamwilishwa katika Mashauri ya Kiinjili na kamwe wasiwe ni Mapadre na Watawa
wasiokuwa na furaha kana kwamba, wameonjeshwa pili pili kichaa! Uzuri wa maisha ya
Kipadre na Kitawa ni ile furaha ya kweli inayojikita katika uaminifu kwa Mungu, Kanisa
na Jirani, kama kielelezo makini cha ushuhuda wa Injili.
Baba Mtakatifu Francisko
anawaalika Waseminari na Wanovisi kushiriki kikamilifu katika Sakramenti za Kanisa
na kwa namna ya pekee Sakramenti ya Upatanisho, inayowaonjesha upendo na huruma ya
Mungu isiyokuwa na kifani. Wasiogope kukiri dhambi zao, ili kujipatanisha na Mungu
pamoja na jirani zao. Hapa kuna haja ya kukazia fadhila ya ukweli na uwazi.
Baba
Mtakatifu Francisko anasema kwamba, katika majiundo ya Kipadre na Kitawa kuna mambo
makuu manne yanayopaswa kuzingatiwa yaani: majiundo na maisha ya kiroho; majiundo
ya kiakili na maisha ya kitume; mambo yatakayowawezesha vijana hao kutekeleza dhamana
na wajibu wao wa kutangaza Injili kwa ari na moyo mkuu kabisa, daima wakitambua kwamba,
wanapaswa kuishi katika Jumuiya. Hizi ni nguzo msingi katika ujenzi wa maisha ya kipadre
na kitawa. Baba Mtakatifu amewaonya Waseminari na Wanovisi kutojiingiza katika mambo
ya umbea kwani wambea hawana bunge!
Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari
yake kwa Waseminari na Wanovisi anawaalika kujikita katika maisha ya sala kama njia
ya kuzungumza na kukutana na Yesu ana kwa ana. Hii ni njia kutoka katika ubinafsi
ili kukutana na wengine katika hija ya maisha.
Anasema kwamba, anatamani kuona
Kanisa ambalo ni la Kimissionari, tayari kusoma alama za nyakati na kujitosa kimaso
maso kwa ajili ya Uinjilishaji wa kina, unaomgusa mtu mzima: kiroho na kimwili, changamoto
kwa vijana kushiriki kikamilifu katika mchakato huu, daima wakionesha uaminifu katika
ile njia iliyooneshwa na Kristo mwenyewe. Wawe ni watu wa sala, tafakari ya Neno la
Mungu na matendo ya huruma; watu wanaotafuta utakatifu wa maisha kwa njia ya Maadhimisho
ya Sakramenti za Kanisa.
Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko aliwaalika Waseminari
na Wanovisi, kila mmoja kusali Sala ya Baba Yetu katika lugha yake mwenyewe, kwani
kwa pamoja wanaunganishwa na Imani katika Kristo na Kanisa lake!
Imehaririwa
na Padre Richard Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.