2013-07-08 12:25:30

Utandawazi usiojali umepelekea watu kushindwa kusikiliza kilio na mahangaiko ya wakimbizi na wahamiaji wanaokufa maji baharini!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 8 Julai 2013 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kisiwa cha Lampedusa, Kusini mwa Italia kama kielelezo cha mshikamano na wakimbizi pamoja na wahamiaji wanaopoteza maisha yao baharini, jambo ambalo limeendelea kujitokeza mara kwa mara, kiasi kwamba, si habari tena kwa vyombo vingi vya habari.

Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza wananchi wa Kisiwa cha Lampedusa na wadau mbali mbali kwa moyo wa upendo na mshikamano kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi ya maisha kisiwani hapo. Amewakumbuka wahamiaji wa dini ya Kiislam ambao wanaanza Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, anawatakia kheri na baraka katika Kipindi cha Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake, alipenda kuasha dhamiri za watu, ili waweze kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya wakimbizi na wahamiaji; kama binadamu wanaweza kukosea, lakini bado wanabaki kuwa ni ndugu zao, wanaopaswa kupendwa na kuheshimiwa. Hii ni changamoto ya kuepuka utamaduni wa kifo, kama ilivyojionesha kwa kiburi cha Kaini aliyetaka kujifananisha na Mungu na matokeo yake akamuua ndugu yake. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanaalikwa kulinda, kutunza na kudumisha kazi ya uumbaji ambayo Mwenyezi Mungu amemkabidhi mwanadamu.

Baba Mtakatifu anasema, ndugu ni mtu yeyote anayehitaji msaada na faraja katika magumu na changamoto anazokabiliana nazo. Mtu anayetamani kuboresha maisha yake kwa kupata ajira na maisha bora zaidi, lakini kwa bahati mbaya, watu hawa wamekumbana na kifo, hawapati fursa ya kupokelewa, kuonja faraja na ukarimu kutoka kwa watu mbali mbali.

Ni watu ambao wamenyanyaswa na kudhulumiwa na watu wanaojihusisha na biashara haramu ya binadamu; ni watu wanaoteseka kutokana na umaskini, lakini mbaya zaidi ni kuona kwamba, kuna kundi kubwa la wahamiaji ambao amefariki dunia wakiwa njiani kuja Barani Ulaya.

Baba Mtakatifu anasema katika mazingira kama haya, watu wengi wanajikosha kwa kunawa mikono kutohusika na damu ya wahamiaji na wakimbizi wanaopoteza maisha yao wakiwa Baharini. Ni mwaliko wa kuwa ni Wasamaria wema kwa kutekeleza wajibu na dhamana katika maisha kama alivyofanya Yesu, kielelezo cha Msamaria mwema. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuondokana na utawandawazi usiojali maisha na mahangaiko ya watu! Mateso yamekuwa ni jambo la kawaida na kwamba, hakuna kinachomgusa mtu!

Baba Mtakatifu anauliza ni nani kati ya watu waliokuwepo pale, aliyeomboleza kutokana na vifo vya wakimbizi na wahamiaji baharini? Watu wanaanza kusahau umuhimu wa maisha, kiasi hata cha kushindwa kusikia kilio cha wale wanaoteseka na kudhulumiwa katika maisha. Watu wanapaswa kusikitishwa na vitendo vinavyoonesha dhuluma na nyanyaso kwa jirani zao.

Baba Mtakatifu anasema, ameadhimisha Liturujia ya toba na upatanisho, kwa kuomba msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu kutokana na kutojali wala kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya ndugu zao wanaopoteza maisha kwa kufa maji baharini.

Baba Mtakatifu ameomba msamaha hata kwa wale wote wanaofanya maamuzi yanayopelekea mateso na mahangaiko ya wakimbizi na wahamiaji, mwaliko wa kusikiliza kilio cha damu na mahangaiko ya wakimbizi na wahamiaji wanaopoteza maisha yao baharini!







All the contents on this site are copyrighted ©.