Onesheni mshikamano wa upendo kwa wakimbizi na wahamiaji!
Haitoshi kuanzisha vituo maalum kwa ajili ya huduma kwa wakimbizi na wahamiaji sanjari
na kufanya maboresho ya huduma msingi inayotolewa kwa watu hawa ambao mara nyingi
wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha.
Jambo la
msingi linasema, Shirika la Wayesuit kwa ajili ya kuhudumia Wakimbizi ni wananchi
Barani Ulaya kufungua mioyo na akili zao, ili kuonesha mshikamano wa upendo na wakimbizi
pamoja na wahamiaji, wanaohitaji kuonjeshwa kwa namna ya pekee faraja na huruma inayosimikwa
katika utu na heshima ya binadamu. Bara la Ulaya likipania linaweza kutekeleza dhamana
hii kwa kiwango cha hali ya juu kabisa!
Ni tafakari ya kina ambayo imefanywa
na Shirika la Wayesuit kwa ajili ya kuwahudumia wakimbizi, wakati huu Baba Mtakatifu
Francisko anapotembelea Kisiwa cha Lampedusa, Kusini mwa Italia, mahali ambapo kimekuwa
ni kielelezo cha matumaini na mahangaiko ya wakimbizi na wahamiaji hasa kutoka Barani
Afrika. Wananchi wa Bara la Ulaya wanayo fursa na uhuru wa kuweza kutembea sehemu
mbali mbali ndani na nje ya Bara la Ulaya. Hii inaonekana kwamba, inawezekana kutoa
nafasi kwa watu wengine pia kuweza kushiriki katika uhuru huu.
Wakimbizi na
wahamiaji ni watu wanaoendelea kutafuta mahali pa kuhifadhi maisha na utu wao kama
binadamu, lakini bado wanakabiliana na vikwazo vingi. Taarifa ya hali ya wakimbizi
Barani Ulaya inabainisha kwamba, wahamiaji waliomba hifadhi Barani Ulaya, bado wanataabika
kupata malazi safi na bora; wengi wao hawana uwezo wa kupata tiba na huduma nyingine
za kijamii na kwamba, wanashinda na njaa kwa mda mrefu.
Kuna baadhi ya miji
ambamo sheria inaitaka miji hii kuhakikisha kwamba, inatoa makazi na malazi kwa watu
hawa, lakini bado hali ni ya kutisha sana. Hawa ni watu wanaolazimika kulala kwenye
Vituo vya Mabas na Treni. Ni watu wanaotanga tanga utadhani kwamba, “dala dala imekatika
usukani”!
Takwimu za Bara la Ulaya zinaonesha kwamba, katika kipindi cha mwaka
2012, wahamiaji 102, 700 walipewa hifadhi katika nchi za Ulaya. Idadi hii inaweza
kuonekana kuwa ni kubwa, lakini ukweli wa mambo hii ni asilimia 0.02% ya idadi ya
wakazi wote wa Bara la Ulaya. Kuna sheria kali zinazosababisha mchakato wa wakimbizi
na wahamiaji kupata vibali kuwa ni ngumu sana na wale wanaobahatika kuvipata, wanajikuta
wakiwa wametengana na familia zao, hali inayoonesha kwamba, kuna udhaifu mkubwa katika
sheria na taratibu za kupata hifadhi ya kisiasa.
Baadhi ya nchi zimejikuta
zikiwaweka wahamiaji na wakimbizi vizuizini, hali inayoonesha jinsi ambavyo binadamu
anavyoweza kunyanyasika na uhuru wake kubezwa na kutwezwa. Shirika la Wayesuit kwa
ajili ya kuwahudumia wakimbizi, limejitahidi kurekebisha hali hizi, lakini bado kuna
mambo mengi yanayopaswa kuboreshwa. Ziara ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko,
kisiwani hapa iwe ni changamoto kwa wananchi wa Bara la Ulaya kuonesha mshikamano
wa upendo unaoongozwa na kanuni auni.
Baada ya miaka mitano ya majadiliano
ya kina, Mashirika ya Yasiyo ya Kiserikali yaliandika taarifa kwa pamoja kuunga mkono,
baadhi ya hatua zilizochukuliwa na Bunge hilo kuhusu hali ya wakimbizi kwa kuzingatia
sheria zinazozingatia msingi wa kibinadamu. Lakini, kuna mambo yanayopaswa kufanyiwa
marekebisho makubwa kuhusu sheria ili kukidhi mahitaji ya hifadhi ya wakimbizi na
wahamiaji Barani Ulaya.
Mashirika haya yanasema kuna haja ya kubadili mfumo
wa kuwaweka wakimbizi na wahamiaji kizuizini, mchakato uyaangalie makundi maalum pamoja
kupata msaada wa kisheria. Mashirika haya nchini Ujerumani yanasema, kuna haja kwa
Serikali za nchi za Ulaya kuonesha mshikamano pamoja na kushirikiana katika kubeba
gharama za kuwahifadhi wakimbizi, hali ambayo wakati mwingine, inapelekea ongezeko
kubwa la kodi.
Hali ya wakimbizi nchini Ugiriki, Italia, Hungaria na Malta
ni tete kiasi kwamba, wakimbizi na wahamiaji wanalazimika kuishi vizuizini kwa muda
mrefu, jambo ambalo ni kinyume kabisa cha sheria za kimataifa.
Mfumo wa sheria
kwa sasa unawafanya wahamiaji na wakimbizi wengi kushambuliwa, kukosa malazi na hatimaye,
kujikuta wakitumbukia katika umaskini. Wakimbizi walindwe na kupata hifadhi, kwani
ni binadamu wenye heshima na hadhi yao! Wahamiaji wapewe fursa ya kuweza kuishi Barani
Ulaya. Hii ndiyo hali halisi ambayo wakimbizi na wahamiaji wanakumbana nayo katika
nchi mbali mbali Barani Ulaya.