2013-07-08 08:40:56

Kama Wamissionari pandikizeni mbegu ya: maisha, afya na faraja kwa wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 7 Julai 2013, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, aliwashirikisha waamini furaha ya kukutana na kusali pamoja na Waseminari na Wanovisi kutoka sehemu mbali mbali za dunia, katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kusali na kuwaombea vijana hawa ambao wanajiandaa kuwa ni Mapadre na Watawa, ili waweze kukua na kukomaza wito wao, ili hatimaye, waweze kuwa kweli ni Wamissionari kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Anakumbusha kwamba, Yesu alikuwa ni Mmissionari mahiri, lakini pia alipenda kuwashirikisha wafuasi wake katika kutangaza Habari Njema ya Wokovu, huku wakiendelea kuwamegea watu upendo, umoja na mshikamano wa watu wa Mungu.

Hiki ndicho kielelezo cha Jumuiya ya Kwanza ya Wamissionari waliokuwa chini ya uongozi wa Kristo mwenyewe, akawafunda na kuwatuma ulimwenguni kote! Hii ndiyo changamoto iliyoko mbele ya Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo, muda unazidi kuyoyoma, kumbe, hakuna wakati wa kupoteza. Wagonjwa wapate tiba kwani Mungu anataka kumponya mwanadamu kutoka katika mateso na mahangaiko yake.

Huu ndio utume unaoendelea kutekelezwa na Wamissionari sehemu mbali mbali za dunia, huku wakipandikiza mbegu ya maisha, afya na faraja kwa wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Hii ni changamoto kwa Wamissionari kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani, jambo la msingi kwa vijana ni kujenga na kukuza ndani mwao moyo, ari na ujasiri sanjari na kusikiliza sauti ya Kristo inayowaita kuwa ni Wamissionari.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, Wafuasi 72 waliotumwa na Yesu, wanawawakilisha: Makleri, Watawa, Makatekista na Waamini walei wanaojitosa kutangaza Injili ya Kristo kwa njia ya huduma: Parokiani, kwa wagonjwa, maskini na wote wanaoteseka; wote hawa wanashiriki kujenga Ufalme wa Mungu, changamoto kwa kila mwamini kujisikia kwamba, anao wajibu wa kuwa Mmissionari na kwamba, anatumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu.

Wafuasi wale walipewa nguvu ya kumshinda Shetani, lakini Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, mdau mkuu wa Uinjilishaji ni Kristo mwenyewe, wengine ni vyombo vyake anavyovitumia, changamoto ya kumwomba Bikira Maria ili awaombee waweze kuwa ni watangazaji bora wa Injili ya Kristo, wakiwa wamesheheni furaha na ujasiri!

Mara tu baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu Francisko aligusia Waraka wake wa kichungaji, Lumen Fidei, Mwanga wa Imani, ulioanza kuandikwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita kwa kufuata tema ya: upendo na matumaini, yeye anahitimisha kwa kuongeza Imani. Hii ni zawadi kwa Familia ya Mungu inayoalikwa kuzama katika mambo msingi ya imani ya Kikristo, ili iweze kuwasaidia kukabiliana na changamoto katika ulimwengu mamboleo. Waraka huu ni nyenzo muhimu hata kwa wale wanaomtafuta Mwenyezi Mungu na maana ya maisha.

Baba Mtakatifu Francisko anauweka Waraka huu chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria, kielelezo makini cha imani, ili aweze kuwasaidia waamini kuvuna matunda yanayokusudiwa na Kristo mwenyewe.

Baba Mtakatifu ametambua uwepo wa Kikundi cha Mahujaji vijana kutoka Roma, kinachojiandaa kwa ajili ya kwenda kwenye Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani huko Rio de Janeiro, Brazil. Amewahakikishia kwamba, hata Yeye mwenyewe anaendelea kujiandaa kikamilifu, ili kwa pamoja waweze kufanya hija kwenye Siku kuu ya Imani.







All the contents on this site are copyrighted ©.