Waseminari na Wanovisi, tumieni vyema kipindi cha malezi, ninyi ni walimu wa imani,
matumaini na mapendo!
Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kichungaji, Mwanga wa Imani, anawaalika
waamini kusikiliza kwa makini mafundisho ya imani, ili waweze kuwa tayari kutikia
wito kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ili kuwamegea wengine zawadi ya imani, inayopaswa
kupokelewa kwa unyenyekevu mkubwa, ili iweze kuwageuza kuwa kweli ni mashahidi amini
wa Kristo na Kanisa lake; tayari kujitosa kimaso maso kutangaza Injili ya Kristo hadi
miisho ya dunia.
Padre Raymond
Saba, Katibu mkuu Idara ya Kichungaji, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika
Maadhimisho ya Siku ya Waseminari na Wanovisi, kama sehemu ya Maadhimisho ya Mwaka
wa Imani anasema, Waseminari na Manovisi wanapaswa kutambua kwamba, wako katika safari
ya malezi yatakayowawezesha kuwa ni walimu wa imani, matumaini na mapendo.
Kipindi
cha malezi katika hatua zake mbali mbali kisaidie kuimarisha uelewa na misingi ya
imani, inayopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha. Walelewa watambua misingi
ya imani na mafundisho ya Kanisa. Kanisa linaalikwa kuwasaidia vijana hawa kutambua
imani ambayo wanapaswa kwanza kabisa: kuiungama; kuiadhimisha, kuimwilisha kwa kuzingatia
amri za Mungu na mwishowe kuisali kadiri ya Kanisa.
Vijana wanaadhimisha Siku
hii katika Mwaka wa Imani, ili watambue kwamba, wao ni wadau wakuu wa ushuhuda wa
imani kwa sasa na wakati ambapo watakuwa ni Mapadre na Watawa.Vijana hawa watumie
vyema kipindi cha malezi na majiundo yao ya maisha ya Kipadre na Kitawa kwa ajili
ya ustawi na maendeleo ya Kanisa kwa sasa na kwa siku za usoni.