2013-07-06 12:01:22

Mahakama kuu Zimbabwe yasema: Uchaguzi mkuu ni hapo tarehe 31 Julai 2013


Jaji mkuu wa Zimbabwe Gofrey Chidyausiku ametangaza kwamba, Mahakama kuu nchini Zimbabwe imeamua uchaguzi mkuu nchini humo ufanyike tarehe 31 Julai 2013 na hivyo kufutilia mbali hoja iliyokuwa imetolewa na Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai aliyekuwa ameomba uchaguzi mkuu kusogezwa mbele kwa majuma mawili zaidi. Jaji mkuu anasema, hakuna mantiki katika hoja hii kwani kama Serikali ya Umoja wa Kitaifa imeshindwa kufanya marekebisho yaliyotakiwa wakati ikiwa madarakani, majuma mawili hatafua dafu!

Bunge la Zimbabwe lilivunjwa rasmi hapo tarehe 30 Juni 2013 ili kujiandaa kwa mchakato wa uchaguzi mkuu utakao wakutanisha Rais Robert Mugabe na Waziri mkuu Bwana Tsvangirai, kama ilivyojitokeza kwenye kinyang'anyiro cha mwaka 2002 na kile cha mwaka 2008. Ikiwa kama Rais Robert Mugabe mwenye umri wa miaka 89 atachaguliwa tena kuingoza Zimbabwe, basi atakuwa ameiongoza nchi hii kwa zaidi ya miaka 33. Kwa sasa vyama vya kisiasa nchini humo vinaendelea na kampeni!







All the contents on this site are copyrighted ©.