2013-07-06 09:37:37

Lengo la hija ya mahujaji kutoka Tanzania


Baba Mtakatifu Francisko katika Barua yake ya kichungaji, katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Mwanga wa Imani, "Lumen Fidei" anasema mwanga wa imani unabubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu na hivyo kumwangazia mwanadamu katika mapito yake. Ni mwanga unaopata chimbuko lake kutoka katika historia ya mambo ya kale, maisha na utume wa Yesu na ni mwanga unaotoa mwelekeo mpya kwa siku za usoni. RealAudioMP3

Padre Beno Michael Kikudo kutoka Jimbo kuu la Dar Es Salaam ni kati ya mahujaji wa kitanzania wanaofanya hija ya kiroho kama sehemu ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani kwa kutembelea: Roma, Lourdes na Nchi Takatifu. Kwa niaba ya mahujaji wenzake anapenda kumshukuru Mungu kwa kufanikisha hija hii tangu katika hatua za mwanzo kabisa hadi walipoondoka, wakafika Roma, Lourdes na kwa sasa wanajiandaa kwenda Nchi Takatifu.

Anasema, lengo kuu la hija hii ya maisha ya kiroho ni kusali na kutafakari Neno la Mungu pamoja na kushuhudia matendo makuu ya Mungu yanayojionesha kwa jicho la imani, kwani wanatambua kwamba, imani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na mwenye imani, huyo anaweza kuona matendo makuu ya Mungu, ndivyo Baba Mtakatifu Francisko anavyoandika kwenye Waraka wake wa kichungaji Mwanga wa Imani. Wanapenda kusali ili kuliombea Kanisa na Tanzania katika ujumla wake, ili iweze kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa.

Padre Beno Kikudo anasikitika kusema kwamba, kwa miaka mingi watanzania waliishi kwa amani, umoja na mshikamano wa kitaifa, lakini kwa wakati huu, watanzania wameanza kugombania fito kutokana na tofauti za kidini, hali ya kipato na nafasi katika jamii; lakini zaidi ukosefu wa fursa za ajira hasa miongoni mwa vijana. Mahujaji wa Tanzania wanaombea amani ili iweze: kulindwa na kudumishwa.

Maadhimisho ya Mwaka wa Imani ni changamoto ya kuifahamu misingi ya imani, ili waamini waweze kuikiri, kuiadhimisha, kuimwilisha na kuisali na hatimaye, waamini hao waweze kutolea ushuhuda wa imani tendaji katika maisha na vipaumbele vyao, hasa wakati huu Kanisa nchini Tanzania linapoadhimisha Jubilee ya miaka 150 tangu Injili ilipotangazwa kwa mara ya kwanza miongoni mwa Watanzania, Wamissionari wakitokea Visiwani Zanzibar, wakatua nanga Mjini Mkongwe wa Bagamoyo na hatimaye, kuenea sehemu mbali mbali za Tanzania.

Mahujaji wanaombea ustawi na maendeleo ya watanzania wote, ili rasilimali iliyopo iweze kutumika barabara kwa ajili ya maendeleo ya wengi, badala ya watu wachache kutaka kujinufaisha na utajiri pamoja na rasilimali ya nchi. Kumbe, hija hii inapania kuombea: amani, imani, ustawi na maendeleo ya watanzania. Mahujaji kabla ya kuanza hija yao, walibahatika kukutana na kuzungumza na Askofu msaidizi Titus Joseph Mdoe wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, aliyewaaga kwa niaba ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.

Askofu msaidizi Mdoe, aliwapongeza mahujaji kwa kuitikia na kukubali kupokea dhamana ya kuhiji kwa niaba ya Familia ya Mungu nchini Tanzania. Hija ni safari ya kiroho inayorutubishwa kwanza kabisa kwa toba na wongofu wa ndani; kwa maisha ya Kisakramenti na Neno la Mungu, bila kusahau matendo ya huruma.

Ni changamoto kwa mahujaji kufungua masikio ya mioyo yao ili kubainisha yale ambayo Mwenyezi Mungu anapenda kuwaambia mintarafu hali, mazingira na watu wanaokutana nao katika hija hii ya maisha ya kiroho, hasa watakapokuwa katika Nchi Takatifu. Hapa ni mahali ambapo imani ya Kikristo inapata chimbuko lake. Mara baada ya hija yao, watambue na kuonja matunda ya hija hii ambayo wanapaswa pia kuwashirikisha jirani zao!







All the contents on this site are copyrighted ©.