2013-07-05 08:08:58

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 14 ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa


Mpendwa msikilizaji, ninakuleteeni ujumbe wa Neno la Mungu katika Dominika ya 14 ya Mwaka C. Ujumbe wa furaha ni huu “furahini kwa kuwa majina yenu yameandikwa mbinguni”. RealAudioMP3

Mpendwa mwana wa Mungu, katika maisha ya kikristu kwaweza kutokea wasiwasi na mashaka ambayo yaweza kuleta mmomonyoko wa imani. Kumbe ndiyo maana Mama Kanisa hukaa karibu na watoto wake akiwaimarisha kwa njia ya Neno la Bwana na kuwashibisha kwa Sakramenti. Jambo la wasiwasi si la leo bali limewatokea hata wana wa Israeli na hasa walipokuwa utumwani.

Basi kwa sababu hiyo Mungu aliye mfariji na mwenye huruma kwa watu wake, anamtuma Nabii Isaya awafariji kwa maneno ya furaha na ya kutia nguvu. Anawaarika akiwaambia washangilie maana ukombozi utawajia. Aguo hili la kupata uhuru linakamilika katika ujio wa Masiha
.
Masiya huyu aliyekuja kwa ajili ya kuleta uhuru na ukombozi kwa watu amejitoa bila kujibakiza kwa njia ya kifo cha msalaba. Ni msalaba huo ambao katika somo la II Mt Paulo anasisitiza juu ya utukufu wake dhidi ya vitu vingine vyote ambavyo vyaweza kuonekana vya maana katika ulimwengu wa leo. Jambo la pili ambalo analikazia katika kutukuza msalaba ni lile la kuwa kiumbe kipya baada ya kupokea ubatizo. Mambo mengine ya tamaduni yanakuja baadaye.

Zaidi ya hayo Mtakatifu Paulo anakemea wale wanaosisitiza kutahiriwa kama njia ya kuwa mkristo, na hivi akazia uhuru kamili katika kuamua kumfuata Bwana katika uhuru ule wa wana wa Mungu. Kanisa likizikiliza Neno la Mungu linaratibisha ujumbe huo pia katika sheria za Kanisa kanuni 219 ya kwamba mkristo anayo haki ya kuchagua kwa uhuru maisha ambayo anajisikia kuwa ameitiwa na Mungu kuyaishi.

Katika kuutukuza msalaba wa Bwana kuna furaha kuu inayozaliwa daima kama zawadi ya wokovu kwa Mkristo. Jambo hili tunalipata katika Injili ya Dominika hii ya 14. Mwishoni mwa Injili Bwana anawaambia wale wafuasi wake 72, furahini kwa kuwa majina yenu yameandikwa mbinguni. Kwa hakika anayefanya kazi anatarajia mwishoni kupata matunda na matunda kwa Mkristo ni hayo ya kuingizwa katika orodha ya watakatifu wa Mbinguni.

Mpendwa siku hizi tunazo simu za vinganjani, ambazo zaweza kutusaidia kuelewa furaha hii ya kuwa katika orodha ya mbinguni. Unapompatia rafiki yako au mtu unayemwamini kuwa ni ndugu, namba ya simu halafu baada ya muda unampigia na anakuuliza wewe nani? Daima unakata tamaa na kujiuliza juu ya uhusiano kama ni wa kweli au vipi?.

Kwa hakika, matarajio yalikuwa kwamba awe ameiingiza namba yako katika simu yake kama kielelezo kidogo cha mapendo. Basi mwinjili akinukuu maneno ya Bwana ataka tuelewe juu ya upendo wa Mungu kwa wanadamu ulivyo mkubwa kupita hata uwezo wetu. Hawa ndugu 72 walikuwa wanafikiria juu ya kutiiwa na pepo lakini Bwana anaonesha jambo kubwa zaidi ya hilo. Bwana anapopokea namba za simu zetu yaani kwa njia ya ubatizo mara anaziingiza katika simu yake na kamwe hazitoki humo mpaka kwa ombi letu rasmi yaani sisi wenyewe kwa uhuru wetu tunaamua kumwacha!

Basi mpendwa mwana wa Mungu, tujiulize sisi majina yetu yameandikwa wapi? Na yameandikwa kwa kalamu ya mti au kwa kalamu ya wino? Je, yameandikwa kwenye vitabu vya wapiga kura au vitabu vya wagonjwa? Je yameandikwa labda katika moyo wa mtu fulani? Kwa hakika yaweza kuwa katika vitabu hivyo lakini haitaweza kutupa furaha ambayo Nabii Isaya na Mwinjili wanatuambia katika Liturujia ya Neno la Mungu. Inafaa yawe yameandikwa katika moyo wa Mmoja anayetupenda kwa Milele yote! Fikiri na kuwaza juu ya Neno Milele Mkristo we! Kwa maana hiyo si katika Agenda za mikutano bali katika moyo wa Mungu.

Ili tuweze kukaa katika moyo wa Mungu zipo kazi na nyajibu za kutekeleza daima kadiri ya Mwinjili. Wajibu wa kwanza ni kusali ili Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika shamba lake. Watakapokuwa wameingia katika shamba lake lazima wapeleke Injili ya Bwana na si mambo yao wenyewe, ndiyo kusema waachane na mambo yanayowachelewesha kufanya kazi ya Bwana. Wanatakiwa daima kupeleka amani na mapendo katika familia na mahali pote pa uchungaji wao. Wanaalikwa kuwatunza wagonjwa na wenye njaa.

Katika kupeleka Neno la Bwana kutakuwa na kukataliwa na hata kupigwa, kumbe, wakumbuke hayo yalimpata Bwana, na hivi waende sehemu nyingine na kazi ya Bwana inasonga mbele. Hawa wenye kukataa watapata mwanga polepole. Kwa kifupi maisha ya kupeleka Habari njema ni kutoa ushuhuda wa maisha katika kuamini kuliko kina na kwa kila siku kama atuaambiavyo Mtakatifu Luka yakuwa msalaba unatakiwa kuchukuliwa kila siku ya maisha yetu.

Mpendwa, tukitenda kwa upendo mkamilifu basi majina yetu yataweza kuandikwa katika moyo wa Mungu na hapa ndipo kuna furaha ya kweli na uzima wa milele.
Nikutakie yote mema katika kujitahidi kupeleka habari njema kwa mataifa ili jina lako lipate kuandikwa katika orodha ya Watakatifu wa mbinguni. Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya C.PP.S








All the contents on this site are copyrighted ©.