Sadaka ya Misa Takatifu asubuhi ni fursa ya Papa kuzungumza na watu wa nyumbani kwake!
Ibada za Misa Takatifu zinazoadhimishwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa asubuhi
na baadhi ya waamini, lakini hasa zaidi na wafanyakazi kutoka Vatican zinalenga kumsaidia
Baba Mtakatifu kuwafahamu walau baadhi ya wafanyakazi wa Vatican na kujenga familia
ambayo inalihudumia Kanisa la Kiulimwengu. Idadi ya waamini
wanaohudhuria Ibada za Misa ya Asubuhi kwa kawaida hazizidi waamini 50 ni kwa ajili
ya utashi wa Baba Mtakatifu mwenyewe na kwamba, si kila mwamini anaruhusiwa kuhudhuria.
Ufafanuzi huu umetolewa hivi karibuni na Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu
wa Vatican baada ya kupokea mamombi kutoka kwa makundi ya waamini walioonesha nia
na utashi wa kuhudhuria Ibada ya Misa Takatifu zinazoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko
kwenye Kikanisa cha Domus Sanctae Marthae kilichoko mjini Vatican. Kutokana na mwelekeo
huu, Ibada hizi haziwezi kutangazwa moja kwa moja kwenye Luninga au kupitia Radio
Vatican. Mahubiri yanayotolewa na Baba Mtakatifu ni tafakari ya moja kwa moja
na ikumbukwe kwamba, Kiitalia si lugha mama ya Baba Mtakatifu Francisko, kumbe kuna
haja ya kuielewa ugumu unaoweza kujitokeza. Kwa kuandika mahubiri yake, hii ingekuwa
pia ni kazi pevu pengine kuweza hata kumnyima uhuru wa Baba Mtakatifu mwenyewe kuelezea
kile ambacho kimemgusa na ambacho angependa kuwashirikisha waamini wakati huo! Hata
hivyo Padre Federico Lombardi anafafanua kwamba, utajiri wa mahubiri ya Baba Mtakatifu
Francisko unapatikana kwa kina na mapana kwenye Gazeti la Kila siku la L’Osservatore
Romano na Radio Vatican inatoa muhtasari wa mahubiri haya. Kituo cha Televisheni cha
Vatican, CTV walau kinajitahidi kutoa muhtasari wa picha na sehemu ya mahubiri ya
Baba Mtakatifu Francisko. Kuna haja kwa waamini kutambua maana ya Maadhimisho binafsi
na yale ya hadhara. Pale ambapo ambapo Baba Mtakatifu anapaswa kuhubiri mbele ya umati
mkubwa wa watu, mahubiri yake yanapaswa kuandikwa na kuhaririwa, lakini anaposali
na kikundi cha ”watu wa nyumbani mwake” anapata fursa ya kuwamegea utajiri wa Neno
la Mungu kadiri Roho wa Bwana anavyomkirimia kwa wakati huo! Padre Federico Lombardi
anahitimisha ufafanuzi huu kwa kusema kwamba, uamuzi huu unaheshimu utashi na matakwa
ya Baba Mtakatifu Francisko pamoja kuwapatia nafaasi waamini wengi zaidi kuendelea
kufaidi mahubiri yake kwa njia za mawasiliano ya kisasa.