2013-07-03 09:59:06

Wanasema, Rais Obama amefunika Tanzania!


Rais Barack Obama wa Marekani amehitimisha ziara yake ya kikazi kwa nchi tatu za Kiafrika, yaani Senegal, Afrika ya Kusini na Tanzania, ambako waswahili wanasema, eti, "amefunika".

Kati ya mambo ambayo yanaendelea kupewa kipaumbele cha pekee na uongozi wa Rais Obama ni uhakika wa usalama wa chakula ili kupambana na baa la njaa linaloendelea kutesa mamillioni ya watu duniani; afya: kwa kupambana na ugonjwa wa Ukimwi na maboresho katika huduma ya nishati ya umeme, ili Bara la Afrika liweze kucharuka katika maendeleo, hatimaye, liweze kuondokana na umaskini.

Katika mapambano dhidi ya baa la njaa, Serikali ya Marekani kuanzia mwaka 2010 imechangia kiasi cha dolla billioni 3.5 ambazo zimesaidia kuokoa maisha ya watu wengi Barani Afrika. Marekani itatoa kiasi cha dolla billioni 7 kwa ajili ya nishati ya umeme. Rais Obama anaendelea kuwachangamostisha Marais wa Afrika kusimama kidete kulinda na kudumisha utawala bora, demokrasia pamoja na kung'oa vitendo vya rushwa na ufisadi ambavyo ni kizingiti kikuu cha maendeleo Barani Afrika.

Rais Obama amewahakikishia wananchi wa Kenya kwamba, wao ni sehemu ya moyo wake na kwamba, iko siku atawatembelea, pengine kwa sasa hali ya hewa bado si shwari sana! Rais Obama amewaalika Marais wa Afrika hapo mwakani, kuhudhuria mkutano unaopania kuimarisha urafiki kati ya Marekani na Afrika katika mchakato wa maendeleo endelevu, kwani wakati wa kutoa hotuba nzuri umekwisha, sasa watu wanataka kuona vitendo!







All the contents on this site are copyrighted ©.