2013-07-03 07:09:20

Vyombo vya habari viwe ni madaraja ya uhusiano mwema kati ya watu!


Baba Mtakatifu Francisko amekipongeza Kituo cha Televisheni cha Vatican, CTV kwa jitihada zake za kuhakikisha kwamba, kinaendelea kuwa ni daraja kati ya Vatican na watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu ameyasema hayo hivi karibuni mara baada ya Kituo cha Televisheni cha Vatican kuwekeana mkataba wa ushirikiano na Kituo cha Televisheni cha “Channel 21”. RealAudioMP3

Wananchi wa Italia na Ulaya kwa ujumla watakuwa na fursa ya kuweza kufahamu hali halisi ya maisha na utume wa Kanisa Bueno Aires. Hii ni kutokana na ushirikiano wa Kanisa Katoliki nchini Italia kwamba, Kituo cha Televisheni cha Jimbo, kinaweza kurusha matangazo yake kwa umati mkubwa zaidi, ili kuweza kufahamu utume na maisha ya Kanisa kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Kwa njia hii, watu wataweza kufahamiana na hatimaye, kubomoa kuta za utengano, ambazo mara nyingi zimekuwepo kati ya watu wa mataifa.

Itakumbukwa kwamba, Kituo cha Televisheni cha Channel 21, kinamilikiwa na kuendeshwa na Jimbo kuu la Buenos Aires na kilianzishwa na Kardinali Jorge Mario Bergoglio kunako mwaka 2004. Baba Mtakatifu ameyasema hayo hivi karibuni alipokuwa anazungumza na Monsinyo Dario Viganò, Mkurugenzi mkuu wa Kituo cha Televisheni cha Vatican.

Akizungumza katika hafla ya kuwekeana mkataba kati ya Kituo cha Televisheni cha Vatican na Kituo cha Televishen cha Channel 21 mjini Vatican, Askofu mkuu Claudio Maria Celli anasema, hizi ni juhudi zinazofanywa na CTV kama sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Miaka thelathini tangu kilipoanzishwa. Ni kituo ambacho kimekuwa kikirusha picha za Mababa Watakatifu: Yohane Paulo wa pili, Benedikto wa kumi na sita na sasa Papa Francisko.

Kituo hiki kinaendelea kuhariri na kuhifadhi picha zote zilizopigwa na Channel 21 wakati wa uongozi wa Kardinali Bergoglio, Jimbo kuu la Buenos Aires, Argentina. Kazi hii inaunganisha pia picha zote za Kardinali Bergoglio hadi tarehe 13 Machi 2013, ambazo zitawekwa katika mfumo wa dijitali.

Hifadhi ya picha hizi inafanikishwa na mradi mkubwa wa Chumba cha kuratibu matangazo, ambacho kwa sasa kina uwezo mkubwa. Chombo hiki kimenunuliwa kutoka kwenye Kampuni ya Sony. Kumbe, hakutakuwa na haja tena ya kutumia mfumo wa picha ambazo zilikuwa zimehifadhiwa kwenye Kanda.

Channel 21, tangu kilipoanzishwa, kimekumbana na changamoto mbali mbali katika kuandaa na kurusha vipindi vyake kwa umati mkubwa zaidi wa wananchi wa Argentina. Viongozi wa Channel 21 kutoka Argentina waliohudhuria katika halfa ya kuwekeana mkataba na Kituo cha Televisheni cha Vatican wanasema, Kardinali Jorge Mario Bergoglio, si mshabiki sana wa masuala ya Televisheni, lakini tangu mwanzo alitambua umuhimu wake katika mchakato mzima wa Uinjilishaji wa mtu mzima: kiroho na kimwili.

Akajifunga kibwebwe kuwekeza katika uanzishwaji wa kituo hiki, leo hii kina mafanikio makubwa. Alitamani kujenga na kuimarisha Kanisa, linaloshirikisha tunu msingi za maisha ya Kikristo, kiutu na kimaadili.

Kwa njia hii, kadiri ya mawazo ya Kardinali Bergoglio, Televisheni ilikuwa na wajibu wa kuwaendea watu waliokuwa pembezoni mwa Jamii, ili kuweza kuwashirikisha ile furaha ya Ujumbe wa Neno la Mungu








All the contents on this site are copyrighted ©.