Hija ya mshikamano na wahamiaji wanaokufa maji baharini!
Baba Mtakatifu Francisko kwa kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya wakimbizi na
wahamiaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaokimbilia Barani Ulaya wakiwa na
tumaini la kupata maisha bora, lakini wanakumbana na kifo maji, Jumatatu, tarehe 8
Julai 2013 atatembelea Kisiwa cha Lampedusa, kilichoko Kusini mwa Italia, kama alama
ya mshikamano wa dhati na watu wote wanaoteseka kutoka na vita, kinzani na majanga
asilia.
Ratiba iliyotolewa mjini Vatican inaonesha kwamba, Baba Mtakatifu
ataondoka kutoka kwenye Kiwanja cha Ndege za Kijeshi, Ciampino majira ya saa 2:00
asubuhi na anatarajiwa kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Lampedusa saa 3:15 na kupokelewa
na Askofu mkuu Francesco Montenegro wa Jimbo kuu la Agrigento pamoja na Mstahiki Meya
Giuseppina Nicolini wa Lampedusa.
Baadaye, Baba Mtakatifu katika safari hii
ya kichungaji kwa mara ya kwanza nje ya Roma atasafiri kwa gari hadi mahali panapojulikana
kama Cala Pisana, hapo atapanda Boti kuelekea Kisiwa cha Lampedusa. Akiwa kisiwani
hapo, ataungana na wavuvi wakiwa kwenye mashua na boti zao kwenda kutupa shada la
maua kwa ajili ya kuwakumbuka wale wote waliopoteza na wanaoendelea kupoteza maisha
yao baharini wakiwa na tumaini la kuokoa maisha yao kutokana na vita, maafa asilia
au migogoro ya kidini, kisiasa na kijamii au wale wanaotamani kuboresha maisha yao
ili kuwa na uhakika wa leo na kesho bora zaidi.
Baba Mtakatifu atawatembelea
na kuzungumza na wahamiaji wanaohifadhiwa kwenye Kituo cha "Punta Favolo". Majira
ya saa 4:00 anatarajiwa kuanza kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na baada ya Misa,
ataondoka na kuelekea kwenye Parokia ya Mtakatifu Gerlando kwa mapumziko mafupi. Saa
6: 45 ataondoka kwa ndege kurudi mjini Roma na hatimaye, Mjini Vatican.