2013-07-03 11:03:56

Adhabu ya kifo imepitwa na wakati!


Kwa sababu uhai wa binadamu ni mtakatifu, Tangu mwanzo wake, unahusisha tendo la Mwenyezi Mungu la kuumba na unabaki daima katika uhusiano wa pekee na Muumba, aliye lengo lake kuu. Kakuna anayeruhusiwa kuangamiza maisha ya mtu kwani. Hili ni tendo zito linalopingana na hadhi ya mtu na utakatifu wa mwenyezi Mungu. Wasio na hatia na wenye haki usiwauwe.

Hivi ndivyo Katekesimu Mpya ya Kanisa Katoliki inavyofundisha na kuendelea kukazia kwamba, adhabu inayotolewa na mamlaka halali ya nchi inalenga kurekebisha vurugu iliyotokana na kosa, kulinda utaratibu wa jamii na usalama wa watu, pamoja na kumsaidia mkosefu kujirudi.

Adhabu inayotolewa inatakiwa ilingane na uzito wa kosa. Siku hizi kutokana na Serikali kuwa na njia za kuzuia makosa ya jinai kwa kumfanya mkosefu asiweze kudhuru, kesi ambazo zinahitaji kabisa adhabu ya kifo "zimekuwa nadra sana, au karibu hazipatikani. Pale ambapo njia ya kutomwaga damu zinatosha, mamlaka iridhike nazo, kwa kuwa zinaendana vizuri zaidi na hali halisi ya ustawi wa jamii. Zinalingana zaidi na hadhi ya binadamu, tena hazimnyimi moja kwa moja nafasi ya kujirekebisha.

Ni kutokana na Mafundisho haya ya Kanisa, Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria, hivi karibuni limelaani kitendo cha Serikali kutekeleza adhabu ya kifo, iliyotokea mjini Benin kuwa ni kitendo cha kinyama dhidi ya utu na heshima ya binadamu. Tangu mwaka 2006 kumekuwepo na mchakato wa kufuta adhabu ya kifo nchini Nigeria, mchakato ambao kwa sasa umevurugwa kutokana na Serikali kuamua kutekeleza adhabu ya kifo kwa wafungwa wanne, hapo tarehe 24 Juni 203.

Askofu mkuu Ignatius Kaigama, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria anasema, hadi sasa adhabu ya kifo inatajwa kwenye Katiba ya nchi, jambo ambalo linapaswa kurekebishwa ili kulinda na kudumisha uhai wa mwanadamu ambayo ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Baraza la Maaskofu linaiomba Serikali kuanzisha mchakato wa kufanya marekebisho ya dhati katika Katiba ili kuondokana na sheria ambazo zinakiuka haki msingi ya mwanadamu, yaani uhai. Adhabu ya kifo imepitwa na wakati kwani haitoi haki kwa mtuhumia kujirekebisha kwa siku za usoni.

Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria linaiomba Serikali kuhakikisha kwamba, inaibua mbinu mkakati utakaowawezesha wafungwa kujirekebisha na hatimaye, kuwa ni raia wema mara baada ya kutumikia vifungo vyao. Leo hii kuna idadi kubwa ya nchi ambazo zinaendelea kufuta adhabu ya kifo kwa raia wake. Lakini watuhumiwa wa makosa mbali mbali wanaendelea kunyongwa nchini China, Iran, Iraq, Falme za Kiarabu na Marekani.







All the contents on this site are copyrighted ©.