2013-07-01 07:21:31

Mzee Nelson Mandela ni mfano na kielelezo cha ushujaa ulimwenguni!


Rais Barack Obama wa Marekani wakati wa ziara yake nchini Afrika ya Kusini, Jumapili tarehe 30 Juni 2013 amewataka vijana Barani Afrika kujifunga kibwebwe ili kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika mustakabali wa maendeleo Barani Afrika, kama walivyofanya akina Mzee Nelson Mandela, aliyekuwa na ndoto ya usawa, haki na fursa sawa kwa wote.

Akihutubia kwenye Chuo kikuu cha Cape Town, Rais Obama amempongeza na kumshukuru Mzee Nelson Mandela ambaye kwa sasa anapambana na mauti, kwamba alionesha ushujaa wa pekee ulioleta mabadiliko makubwa katika ulimwengu. Anawataka vijana kusimama kidete kupinga dhuluma na nyanyaso Barani Afrika. Afrika inao wajibu wa kukamilisha ndoto zilizoanzishwa na viongozi mashuhuri Barani Afrika kama akina Mzee Nelson Mandela, kwa kutetea: uhuru, mafao na ustawi wa wengi.

Rais Obama amesema kwamba, Marekani itawekeza kiasi cha dolla billioni saba katika nishati ya umeme Barani Afrika. Nchi ambazo zinatarajiwa kufaidika na msaada huu ni Ethiopia, Ghana, Kenya, Liberia na Tanzania. Lengo kuu ni kuhakikisha kwamba, Bara la Afrika linaendelea kucharuka katika maendeleo. Lakini ameonya kwamba, Marekani itahakikisha kwamba, inatetea utu na heshima ya watu Barani Afrika, kwa kuunga mkono juhudi za kufufua uchumi, amani na demokrasia.

Marekani itasaidia juhudi za Bara la Afrika katika kupambana na ugonjwa wa Ukimwi, kwa kutoa dawa za kurefusha maisha pamoja na kupunguza maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutoka kwa Mama kwenda kwa mtoto wakati wa kujifungua. Serikali ya Marekani inatarajia kutumia kiasi cha dolla za kimarekani billioni 4.2 katika mradi huu.

Rais Obama alifanikiwa kukutana na kuzungumza na Askofu mstaafu Desmond Tutu wa Kanisa Anglikani Afrika ya Kusini, aliyesimama kidete kupinga sera za ubaguzi wa rangi nchini humo. Rais Obama ametembelea Kisiwa cha Robben, mahali ambako Mzee Nelson Mandela aliishi kama mfungwa kizuizini kwa muda wa miaka kumi na minane, kati ya miaka ishirini na saba aliyoishi kifungoni nchini Afrika ya Kusini.

Akiwa gerezani humo, ambako ametumia takribani dakika ishirini kulitembelea amesema, kwa niaba ya Familia yake, kwa unyenyekevu mkubwa ametembelea mahali ambapo watu wenye ujasiri walikumbana uso kwa uso na ukosefu wa haki msingi za binadamu bila kukata tamaa. Dunia inawashukuru mashujaa waliofungwa Kisiwani hapo na kwamba moyo wa binadamu una nguvu zaidi. Haya ni kati ya maneno yaliyoandikwa na Rais Obama kwenye kitabu cha wageni kwenye Kisiwa cha Robben. Rais Obama amekwisha tembelea Senegal, Afrika ya Kusini na Jumatatu anatinga nchini Tanzania.







All the contents on this site are copyrighted ©.