Dar es Salaam hapatoshi: Rais Obama na Bush wametinga timu!
Rais Barack Obama wa Marekani na Rais mstaafu George Bush wa Marekani wako nchini
Tanzania kwa shughuli tofauti. Rais mstaafu Bush yuko nchini Tanzania ili kushiriki
katika mkutano wa Taasisi yake unaopania kuwajengea uwezo wanawake katika sekta ya
elimu, afya na uchumi na maendeleo. Rais mstaafu Bush anatarajiwa kuzungumza na wanawake
kutoka Tanzania, Jumanne, baada ya Rais Barack Obama kuhitimisha ziara yake nchini
Tanzania.
Wachunguzi wa masuala ya kisiasa wanasema, uwepo wa Rais Obama na
Bush kwa pamoja Jijini Dar es Salaam ni kielelezo makini kwamba, Marekani inawajali
wananchi wa Afrika na wanataka kusaidia katika mapambano dhidi ya ujinga, maradhi
na umaskini. Itakumbukwa kwamba, Rais mstaafu George Bush alisaidia sana katika mapambano
dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi Barani Afrika, juhudi zinazoendelezwa na Rais Obama.
Akizungumza
na waandishi wa habari, Rais Obama amesikika akisema kwamba, ukata na sera za Marekani
zinamnyima uhuru wa kuweza kulisaidia Bara la Afrika, lakini msaada unaotolewa na
Marekani kwa sasa unaweza kuleta mabadiliko makubwa kwa wananchi wa Afrika.