Yaliyojiri katika maisha na utume wa Papa Francisko!
Miezi kadhaa imekwisha yoyoma tangu Papa Francisko alipochaguliwa kuliongoza Kanisa
Katoliki. Watu wengi wameguswa na maneno, matendo na ushuhuda wake wa kazi za kichungaji,
jambo ambalo limewaacha wengi wakiwa wameshikwa na bumbuwazi, kwani kwao, matukio
haya yote ni kama kielelezo cha ari na mwamko mpya wa Injili ya Kristo, inayojikita
katika Uinjilishaji mpya.
Waamini wanakumbushwa
kwamba, Yesu anaendelea kuliongoza Kanisa lake kwa njia ya Roho Mtakatifu na kwamba,
watu wengi ambao wamekata tamaa kutokana na magumu na shida mbali mbali za maisha,
wanasubiri kusikia ujumbe wa matumaini ukitangazwa mioyoni mwao.
Haya ndiyo
yanayojitokeza mjini Vatican, kwa kuona umati mkubwa wa watu kutoka sehemu mbali mbali
za dunia wakienda kumsikiliza, kumwangalia na kukutana na Baba Mtakatifu Francisko
ambaye kwa miezi ya hivi karibuni amekuwa ni gumzo la vyombo vya habari kitaifa na
kimataifa!
Ni maneno ya Monsinyo Piero Coda, Mwanataalimungu na Jalim kutoka
Chuo Kikuu cha Sophia anayechambua kwa kina na mapana matukio mbali mbali yanayoendelea
kujiri katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko. Ni kiongozi ambaye amepokelewa
vyema katika medani mbali mbali za maisha na hivyo kuwasha moto wa matumaini kwa wale
waliokuwa wamekata na kujikatia tamaa ya maisha. Amewagusa waamini na wasioamini kutokana
na maneno na matendo yake ya kila siku.
Baba Mtakatifu Francisko ameonesha
unyenyekevu wa Mama Kanisa unaogusa mioyo ya watu na kuacha chapa ya kudumu, kama
vile Yesu mwenyewe alivyotenda alipokuwa hapa duniani. Amewagusa walimwengu waliokuwa
wameelemewa na kumezwa na malimwengu, lakini bado wana kiu ya kutaka kumfahamu Mungu
kutoka katika undani kabisa wa mioyo yao! Huu ni mwamko mpya wa Uinjilishaji Mpya,
ambao ni mapambazuko ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko
anayefanya hija pamoja na Familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia, ni sawa na
mkate unaomegwa kwa ajili ya wengi! Ni kiongozi anayeshirikisha ujumbe na changamoto
za Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha
Mwaka wa Imani, chemchemi mpya ya imani na matumaini kwa wengi!
Baba Mtakatifu
Francisko anatambua dhamana yake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, anayepaswa kushirikiana
kwa karibu zaidi na Maaskofu mahalia waliotawanyika sehemu mbali mbali za dunia, kama
sehemu ya utekelezaji wa dhamana na majukumu yake kama Kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki.
Anaendelea kukazia umuhimu wa Sinodi za Maaskofu kama kielelezo cha umoja na mshikamano
wa Kanisa katika kupembua, kupanga na kutekeleza mikakati ya shughuli za kichungaji
pamoja na kuendelea kusoma alama za nyakati.
Moyo wake wa unyenyekevu umemwezesha
katika miezi ya uongozi wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kupendwa na kukubalika
na wengi. Watu bado wanakumbuka ile siku ya kwanza alipoinamisha kichwa chake, akiomba
sala kutoka kwa waamini; wazo ambalo ameliendeleza kwa nyakati tofauti tofauti anapokutana
na watu. Hili ni tukio la kihistoria litakalobaki katika historia kwa kipindi cha
miaka mingi.
Monsinyo Piero Coda anasema, mchakato wa Uinjilishaji Mpya umepata
chimbuko lake katika Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican; ukavaliwa njuga na Papa Paulo
wa sita, aliyelihamasisha Kanisa kuuinjilisha ulimwengu; dhana iliyofanyiwa kazi kwa
kina na mapana na Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili aliyezunguka sehemu mbali mbali
za dunia, akiwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumfungulia Kristo malango
ya maisha yao bila woga.
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita,
akawaandaa waamini kwa mafundisho tanzu yenye kina na hivyo huu ukawa ni mwendelezo
wa mkate wa uzima wa milele unaoendelea kumegwa kwa ajili ya wengi katika uhalisia
wa maisha. Uinjilishaji Mpya unalitaka Kanisa kuonesha mwelekeo mpya katika kuishi
na kimwilisha maisha na utume wake, kama anavyofanya kwa sasa Baba Mtakatifu Francisko!.