2013-06-29 08:45:36

Upadre ni mwaliko wa furaha, huduma na uhusiano wa dhati na Kristo pamoja na Kanisa lake!


Mimi ni Padre ninafurahia wito na maisha yangu ya Kipadre, yaani we acha tu! Hili ndilo jibu makini linalopaswa kutolewa na kila Padre kwa kutambua kwamba, wito wa Kipadre ni mwaliko wa furaha, huduma kwa ajili ya Familia ya Mungu inayopaswa kujengeka katika uhusiano wa dhati na Kristo kwa njia ya: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na Matendo ya Huruma.

Katika ulimwengu mamboleo, kuna mashindano makubwa ya kutafuta mafanikio ya haraka haraka na kila mtu anataka kujijenga, kupata mali na utajiri mkubwa. Kwa Mapadre hii ni changamoto kubwa na endelevu, hasa kwa kutambua kwamba, wao wanapaswa kujitosa kimasomaso bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na Kanisa; ili kuwamegea jirani zao imani kwa Kristo na Kanisa lake. Kwa mantiki hii, wito na maisha ya kipadre inakuwa ni hija ngumu na yenye changamoto; hija inayobubujika furaha na matumaini; ni wito ambao wakati mwingine unawaacha watu wengi wakiwa wamepigwa na butwaa, lakini jambo la kushangaza unatafutwa na wengi!

Kuna uwezekano wa kukua na kukuza wito wa Kipadre kwa kutambua kwamba, hii ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu; zawadi inayokua na kukomaa katika Jumuiya ya Waamini. Jumuiya za Kikristo hazina budi kuwa ni mahali ambapo furaha ya maisha na wito wa Kipadre inabubujika bila ukomo! Ni dhamana ya Padre mwenyewe kuhakikisha kwamba, anapalilia mazingira ya kuishi upadre wake kwa moyo wa furaha.

Hizi ndizo changamoto zinazofanyiwa kazi na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Ulaya, (CCEE) kuanzia tarehe Mosi, Julai hadi tarehe 4 Julai 2013 katika Kongamano la Miito ya Kipadre mjini Roma. Kongamano hili linahudhuriwa na wajumbe kutoka Tume za Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya zinazojihusisha na miiti ya Kipadre. Wawakilishi wa Mashirika ya Kitawa pia watashiriki na kuna wawakilishi kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, nao pia wanashiriki.

Wajumbe watapata fursa ya kuweza kupembua wito na maisha ya Kipadre mintarafu mwanga wa Waraka kutoka Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki kuhusu mwelekeo wa shughuli za kichungaji kwa ajili ya kuhamasisha miito ya Kipadre, uliotolewa kunako Mwaka 2012. Mkutano huu unahudhuriwa pia na Kardinali Mauro Piacenza na Askofu mkuu Celso Morga Iruzubieta, Mwenyekiti na Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makleri.

Itakumbukwa kwamba, kunako tarehe 16 Januari 2013, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, alifanya mabadiliko makubwa kwa kuhamisha mambo ya majiundo ya Mapadre kutoka katika Baraza la Kipapa la Elimu na kulikabidhi Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makleri. Kongamano hili litakuwa ni fursa makini kwa wajumbe na mabingwa wa maisha na wito wa kipadre kuweza kubadilishana uzoefu na mang'amuzi hasa kwa kuzingatia kwamba, Mama Kanisa kwa sasa anayaelekeza macho yake kwenye Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani. Haya ni matukio ambayo yanaweza kuwasaidia vijana kukuza na kukomaza wito wa Kipadre.







All the contents on this site are copyrighted ©.