IMBISA na mchakato wa uchaguzi mkuu nchini Zimbabwe
Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika, IMBISA, hivi karibuni
lilimtembelea na hatimaye, kuzungumza na Rais Josè Eduardo Dos Santos wa Angola kuhusu
hali ya kisiasa Kusini mwa Afrika na kwa namna ya pekee, mchakato wa uchaguzi mkuu
nchini Zimbabwe.
Hizi ni juhudi za IMBISA kukutana na kuzungumza na viongozi
wakuu wa Serikali Kusini mwa Afrika, kama sehemu ya mbinu mkakati unaopania maboresho
ya utawala bora, demokrasia, haki, amani na upatanisho wa kweli, kwa ajili ya ustawi
na maendeleo ya wananchi wanaoishi Kusini mwa Afrika. Itakumbukwa kwamba, wajumbe
wa IMBISA wamekwisha kutana na kuzungumza na Rais Armando Guebuza wa Msumbiji. Ujumbe
wa IMBISA ulikuwa chini ya uongozi wa Askofu Antonio Jaca Caxito wa Angola.
IMBISA
inawataka viongozi wa SADC kuhakikisha kwamba, wanafanikisha uchaguzi mkuu nchini
Zimbabwe na kwamba, uchaguzi huu unakuwa ni huru na wa haki. Malumbano ya viongozi
wakuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa si dalili njema kwa ustawi na maendeleo ya wananchi
wa Zimbabwe na Afrika katika ujumla wake.
Ujumbe wa IMBISA pia umeonesha wasi
wasi kutokana na kinzani zinazoanza kufuka moshi kati ya Serikali na Chama cha Upinzani
cha RENAMO, wanaotaka kurudi tena msituni kuendesha mapambano ya silaha nchini Msumbiji.