2013-06-28 14:15:23

Wakristo wanachangamotishwa: kutafuta, kujenga na kuimarisha umoja; ili kuzima kiu ya ukweli, upendo, matumaini, umoja kwa njia ya ushuhuda!


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 28 Juni 2013 amekutana na kuzungumza na ujumbe kutoka kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli ambao uko mjini Roma ilikushiriki katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani, inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 29 Juni.

Baba Mtakatifu anasema hiki ni kielelezo cha imani katika matumaini na upendo kati ya Makanisa haya mawili, utamaduni ambao ulianza kunako mwaka 1969, kwa kutembeleana wakati wa Maadhimisho ya Watakatifu Petro na Paulopamoja na ile ya Mtume Andrea. Anamshukuru kwa namna ya pekee Patriaki Bartolomeo wa kwanza na Sinodi kwa kutuma wawakilishi katika tukio hili.

Baba Mtakatifu bado anakumbuka lile tukio la kihistoria, wakati Patriaka Bartolomeo wa kwanza alipoamua kwa m ara ya kwanza katika historia ya Kanisa kushiriki katika Ibada ya mwanzo wa utume wa Papa Francisko kama Askofu wa Roma na sasa uwepo wao kwa tukio hili bado ni kielelezo cha mwendelezo wa furaha ile.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kwamba, Wakristo kwa pamoja wanaendelea kuchangamotishwa kutafuta, kujenga na kuimarisha umoja miongoni mwao ili kuweza kuzima kiu ya ukweli, upendo, matumaini, umoja; unaojionesha kwa namna ya pekee katika ushuhuda wa maisha ya umoja na mshikamano miongoni mwa Wakristo, ambao kwa pamoja wanatumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu na kuadhimisha Mafumbo ya maisha mapya ya Kristo.

Baba Mtakatifu anasema, Kanisa linatambua kwamba, umoja ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ambao kimsingi waamini wanaalika kuutafuta kwa njia ya sala sanjari na kuandaa mazingira ambamo zawadi na neema hii inaweza kupokelewa. Mchakato huu unejionesha wazi katika Tume ya Ushirikiano wa Kimataifa katika majadiliano ya kitaalimungu inayosimamiwa na Kardinali Kurt Koch na Askofu mkuu Ioannis. Tayari Tume hii imekwisha chapisha charaka mbali mbali na sasa inashughulikia suala nyeti kati ya taalimungu na ufahamu wa Kanisa; Kiongozi mkuu na Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, ni jambo la msingi kuona kwamba, Makanisa haya mawili yanajadiliana kwanza kabisa yale mambo msingi yanayowaunganisha kwa pamoja kama Wakristo pamoja na kuangalia yale ambayo bado yanawatenganisha. Hapa kuna haja ya kufahamu kwa undani Mapokeo na kuyathamini. Hapa Baba Mtakatifu anasema, umoja na mshikamano miongoni mwa Maaskofu Katoliki na Sinodi kwa Kanisa la Kiorthodox. Majadiliano haya makini yataweza kutoa matunda yake kwa wakati muafaka.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, anafarijika kusikia kwamba, waamini wa Makanisa haya mawili wanatambua na kuthamini dhana ya majadiliano inayopania kuufikia ukweli ambao Kristo ameliachia Kanisa lake na kazi inayoendelea kutekelezwa na Roho Mtakatifu. Kutokana na mwelekeo huu, hakuna haja kwa waamini kuogopa kukutana na kujadiliana katika ukweli na kwa kuongozwa na Roho Mtakatifu waweze kufikia ukweli mkamilifu.

Baba Mtakatifu katika hotuba yake amewakumbuka pia Wakristo wanaoendelea kudhulumiwa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake; bila kuwasahau maskini. Anawaomba waendelee kumsindikiza kwa sala, ili Kristo aweze kumsaidia katika kutekeleza utume na maisha yake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.







All the contents on this site are copyrighted ©.