2013-06-28 08:07:12

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya kumi na tatu ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa


Karibuni mpendwa msikilizaji wa Neno la Mungu tunapotafakari pamoja Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 13 ya Mwaka C. Bwana wetu Yesu Kristo katika Injili anatangaza upendo mkamilifu na utume wake wa kuwakoa watu kinyume na fikira za kibinadamu. RealAudioMP3

Mwanadamu hufikiria mara moja kunakokuwa na kinzani, kuangamiza na hasa akiwa na nguvu zaidi ya mpinzani wake. Kristu anapingwa na kunyanyaswa katika nchi iliyo yake na wanafunzi wake wanapendekeza maangamizi dhidi ya wapinzani. Akitambua udhaifu wao anasema Mwana wa Adamu hakuja kuangamiza roho za watu bali kuwaokoa watu na kuwapeleka mbinguni.

Akiendelea katika utume wake anakutana na matukio mbalimbali na anatoa majibu ya kimungu. Tunamwona mtu mmoja akifikiri kumfuasa Bwana ni raha msitarehe anamwomba Bwana akae katika msafara, Bwana akijua hila yake anasema kama wataka kunifuata yakupasa kuwa tayari kulala hata nje katika baridi na maana yake kuwa tayari kutoa maisha yako kwa sababu ya Injili.

Wanaposonga mbele anakutana na mtu mwingine anamwambia nifuate, mtu huyo anaweka kikwazo cha kwanza kumzika Baba yake. Bwana anasema waache wafu wazike wafu wao. Katika hili anataka mmoja ajitoe kikamilifu katika kuhudumu Injili yake si kuanza kubabaika katika maisha mengine yasiyoambatana na Injili ya Bwana. Vivyo hivyo anakutana na mtu mwingine anayeweka kikwazo cha kuwaaga wazazi na ndugu zake. Bwana anasema yakupasa kuangalia mbele daima. Neema ya Mungu yatosha kwa ajili ya ndugu zako.

Mfululizo wa watu mbalimbali wenye vikwazo mbalimbali wanaokutana na Bwana ni kielelezo cha maisha ya wito katika Kanisa. Mara kadhaa watu mbalimbali huweka vikwazo kwa sauti ya Mungu na hasa kwa sababu ya sauti nyingine zuizi. Kumbe ni vema kuzama katika tafakari ili kupambanua sauti ya Mungu na kuitika mpango wa Mungu kadiri ulivyopangiwa. Jambo la pili wito si lelemama, ni jambo la kukaza uso gumegume ukielekea Yerusalemu, ni kushika njia ya msalaba, ni utumishi na si kutumikiwa. Ni kufuatilia mpango wa kichungaji wa Bwana wetu Yesu Kristo.

Mpendwa mwanatafakari ndiyo kusema mpango wa kichungaji wa Bwana ni kuokoa watu walio katika taabu ili waungane na walio katika neema. Ni kuendeleza mpango wa Mungu tangu uumbaji aliposema kila kitu ni chema. Kumbe, kuangamiza watu au viumbe vingine ni kwenda kinyume na mpango wa Mungu. Kristo ni mkombozi na si mwangamizi, Kristo ni mwalimu na mzazi apendaye maisha ya watoto wake yashamiri na kusonga mbele mpaka mwisho wa dahari. Kristo anapoita ili kumfuata ni lazima kuondokana na uzembe na ulegevu usio na msingi wa imani.

Mara kadhaa inajitokeza baadhi ya washika ofisi za Kanisa kuwa wavivu na watu wanaodeka, katika Injili ya leo Bwana anakemea jambo hilo akisema mbweha wana mahali pakuweka vichwa vyao lakini Mwana wa Adamu hana! Ni lazima mpendwa msikilizaji kujikana na kujikatalia katika maisha ya kumfuasa Bwana.

Mtakatifu Paulo akitafakari Neno la Bwana anawaambia Wagalatia kuwa Bwana ametuweka huru na hivi kwa nini tunaswe tena chini ya kongwa la utumwa? Yatupasa kuondokana na vikwazo hivyo vinavyo komaza mwendelezo wa ulaghai na uvivu wa kumtumikia Mungu. Katika somo la kwanza tunapata habari ya Elisha anaitwa na Mungu na mara anaacha mali yake na kuanza safari ya utumishi kwa ajili ya wokovu wa watu. Kwa namna ya Elisha nasi twapaswa kuchangamkia wito wetu tulioupokea wakati wa Ubatizo. Mpendwa Ubatizo si lelemama bali ni wajibu msingi na wa kwanza katika maisha yako. Unapaswa kuupalilia daima ili kwao ukafike mbinguni.

Nikutakie yote mema ukichuchumalia baraka za Mungu na neema zake kwa ajili ya kutengeneza wito wako. Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.