Pallio Takatifu ni alama ya Kristo mchungaji mwema, anayemtafuta Kondoo aliyepotea
ili aweze kumbeba mabegani mwake!
Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo
miamba wa Imani, Jumamosi asubuhi, tarehe 29 Juni 2013, anatarajiwa kuongoza Ibada
ya Misa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican pamoja na kutoa Pallio
Takatifu kwa Maaskofu wakuu, 34 na kati yao kuna 3 kutoka Barani Afrika. Askofu mkuu
Francois Xavier Le Van Hong kutoka Vietnam atapelekewa Pallio Takatifu Jimboni mwake.
Ibada
ya kuwavika Maaskofu wakuu Pallio Takatifu ni ile iliyofanyiwa marekebisho na kuidhinishwa
na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita kunako mwaka 2012. Ibada hii imefupishwa
ili kutoa nafasi kwa waamini kuweza kushiriki kikamilifu katika Maadhimisho ya Ibada
ya Misa Takatifu bila kukatishwa katishwa!
Ibada ya kuwavika Maaskofu wakuu
Pallio Takatifu, itaanza kwa kusomwa orodha ya majina ya Maaskofu wakuu wapya na baadaya
hapo utafuatia wimbo wa kuingilia na baadaye, Kardinali atawatambulisha Maaskofu wakuu
kwa Baba Mtakatifu, ili awapatie Pallio takatifu kielelezo cha ukuu wa Majimbo Makuu
wanaoyaongoza na Utii na Umoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Maaskofu wakuu
wapya watakula kiapo cha utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Pallio Takatifu zitabarikiwa
na baadaye Maaskofu wakuu watavishwa na Ibada ya Misa Itaendelea kwa wimbo wa Bwana
utuhurumie. Ikumbukwe kwamba, hii si Ibada ya Kisakramenti ambayo kimsingi inafanywa
mara baada ya mahubiri, kama inavyojionesha wakati wa kupokea Sakramenti ya Ubatizo,
Kipaimara, Ekaristi Takatifu au Upadrisho.
Kimsingi Pallio Takatifu ni kitambaa
cha sufu safi kinachoshonwa kwa mikono. Mwanzoni ilimaanisha kuwa ni Kondoo aliyepotea;
ni alama pia ya Kristo mchungaji mwema. Ni alama iliyoanza kutumika kunako Karne ya
nne, nyakati za uongozi wa Papa Gregori wa Saba, wakati ambapo Maaskofu wakuu walikuwa
wanafika mjini Roma kwa ajili ya kupokea Pallio Takatifu.
Papa Paulo wa sita,
akafanya marekebisho makubwa, Pallio takatifu ikaanza kutolewa kwa Maaskofu wakuu
wa Majimbo makuu tu!