Askofu Joseph Mbatia wa Jimbo Katoliki la Nyahururu, Kenya, amewataka waamini wanaoishi
nje ya Majimbo yao kuhakikisha kwamba, wanasaidia kuchangia mchakato wa ustawi na
maendeleo ya Majimbo yao na kamwe wasisahau walikotoka. Hii ni changamoto ya kuendelea
kuchangia kwa hali na mali maendeleo ya maeneo walikotoka.
Askofu Mbatia ameyasema
hayo hivi karibuni wakati alipokuwa anaadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwa ajili
ya waamini wanaotoka Jimbo Katoliki la Nyahururu, nchini Kenya kwenye Kikanisa cha
Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Mtakatifu Paulo, Kilichoko mjini Nairobi.
Askofu
Mbatia alitumia fursa hii kufafanua baadhi ya miradi iliyoibuliwa na Jimbo Katoliki
Nyahururu kama sehemu ya mchakato wa kutaka kujitegemea na kulitegemeza Kanisa katika
maisha na utume wake, hasa wakati huu, wanapoendelea kusonga mbele kwa imani na matumaini
ya kusimama kwa miguu yao wenyewe ili kupunguza ufadhili kutoka nje ya nchi.
Jimbo
limebuni mradi utakaogharimu kiasi cha shilingi million 140 hadi utakapokamilika;
mradi ambao kila mwanajimbo anaalikwa kuchangia ndiyo maana anawaalika waamini kutoka
Jimboni humo kushirikishi kikamilifu katika kuchangia kwa hali na mali.
Askofu
Mbatia anawaalika waamini kujiwekea akiba mbinguni kwa njia ya sadaka na matendo ya
huruma kwa jirani na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Anawakumbusha kwamba,
hapa duniani, kila mtu ni mpita njia!