Wakati wananchi wa Afrika ya Kusini na wapenda amani kutoka sehemu mbali mbali duniani
wanapoendelea kuyaelekeza masikio yao nchini Afrika ya Kusini kutokana na hali ya
Mzee Madiba kuendelea kudhohofu zaidi, Rais Barack Obama wa Marekani, katika safarai
yake ya kikazi Barani Afrika, anatarajiwa kutembelea Afrika ya Kusini mwishoni mwa
Juma.
Ratiba inaonesha kwamba, Rais Obama atatembelea Johannesburg na Cape
Town, Jumamosi na Jumapili. Serikali ya Afrika ya Kusini hajazungumzia kuhusu mabadiliko
ya ratiba hii kutokana na kudhohofu kwa Rais Mstaafu Nelson Mandela. Wananchi wa Afrika
ya Kusini wanasema, kwa sasa wanamwachia Mwenyezi Mungu maisha ya Mzee Madiba atende
kadiri ya mapenzi yake.
Hata ikiwa kama atafariki, lakini wananchi wa Afrika
ya Kusini wanapaswa kusherehekea zawadi ya maisha ambayo Mwenyezi Mungu amemkirimia
Mzee Madiba ambaye ameonja, magumu na raha za dunia. Miaka 27 ya taabu na mateso kizuizini
si haba! Miaka 5 ya uongozi kama Rais, ni neema na baraka!
Rais Obama amewasili
mjini Dakar, Senegal tarehe 26 Juni 2013 na atakuwemo nchini humo hadi tarehe 28 Juni
2013 atakapoanza safari yake kuelekea Afrika ya Kusini na Tanzania, wakati huu anapofanya
ziara rasmi kwa ajili ya kutembelea Bara la Afrika.