Mshikamano wa upendo na maskini kutoka sehemu mbali mbali za dunia!
Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani linawaalika waamini kuunga mkono jitihada za
Baba Mtakatifu Francisko za kutaka kuonesha mshikamano wa upendo na maskini pamoja
na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kwa njia ya sadaka na majitoleo yao.
Itakubukwa
kwamba, Maadhimisho ya Siku kuu ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani hapo
tarehe 29 Juni kila mwaka, waamini wanaalikwa kuonesha mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu
Petro kwa kutoa mchango, unaomwezesha Baba Mtakatifu kuonesha mshikamano wa upendo
na maskini pamoja na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.
Baba Mtakatifu
Francisko anapenda kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini wa hali na kipato katika
maisha na utume wake, changamoto kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kumuunga mkono.
Nchini Marekani, waamini watakusanya mchango wao kuanzia Jumamosi tarehe 29 hadi 30
Juni 2013, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Iweni mahujaji wa upendo”.
Kwa njia
hii, waamini wataweza kushiriki katika mchakato unaopania kuwashirikisha wengine upendo
unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Sadaka ya siku hii inawawezesha waamini
kuonja shida na mahangaiko ya jirani zao kutoka sehemu mbali mbali za dunia anasema
Askofu mkuu Dennis Schnurr, Mwenyekiti wa michango, Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani.
Anakumbusha kwamba, haba nah aba hujaza kibaba! Kila mwamini akichangia kwa
moyo wa ukarimu na upendo, mchango unakuwa mkubwa kiasi ambacho Kanisa linaweza kugharimia
mikakati ya maendeleo na shughuli za kichungaji kwa: waathirika wa vita, majanga asilia,
madhulumu ya kidini pamoja na kuendelea kugharimia majiundo ya Makleri, Watawa na
Makatekista, wadau wakuu wa Uinjilishaji Mpya.
Baba Mtakatifu Francis katika
Maadhimisho ya Siku kuu ya Pasaka kwa Mwaka 2013 aliwaalika waamini kuwa kweli ni
mawakala wa huruma ya Mungu kwa kuwa ni vyombo ambavyo vitaweza kutumiwa na Mwenyezi
Mungu kwa ajili kulowanisha dunia, kulinda na kutunza mazingira; kudumisha na kuendeleza
misingi ya haki, amani na upatanisho wa kweli.