Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani, hivi karibuni
alihudhuria mkutano uliokuwa umeandaliwa na Taasisi ya Lumen Christi
ya Chuo Kikuu cha Chicago, Marekani ili kujadili pamoja na mambo mengine athari za
utandawazi katika nchi zinazoendelea, njia madhubuti zinazopaswa kuchukuliwa na Jumuiya
ya Kimataifa katika kujenga uchumi unaokubalika kimaadili.
Kardinali Turkson
anabainisha kwamba, Kanisa lina dhamana na wajibu wa kuwakumbusha viongozi wa kimataifa
kwamba, maskini duniani wanapaswa kuheshimiwa, kuthaminiwa na kusaidiwa ili kuweza
kukabiliana na changamoto mbali mbali za maisha kwa njia ya mshikamano unaoongozwa
na kanuni ya auni; utu wa mtu na maadili vikipewa kipaumbele cha kwanza.
Mama
Kanisa anapozungumza masuala mbali mbali yanayomgusa mwanadamu, kwa kawaifa anawaelekea
watu wote wenye mapenzi mema, kama ilivyokuwa katika Mafundisho ya Waraka wa Papa
Yohane wa Ishirini na tatu, Pacem in Terris, Amani Duniani.
Kardinali
Turkson anasema, Mafundisho Jamii ya Kanisa ni amana na utajiri mkubwa unaopata chimbuko
lake katika miaka 1891 kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa: maisha, utu na heshima
ya binadamu. Ni mafundisho yanayobubujika kutoka katika majadiliano kati ya imani
na akili ya mwanadamu, ili kumuenzi mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Mafundisho haya yanajikita kwa namna ya pekee katika haki, amani, upendo na upatanisho.
Ni mafundisho ambayo yanajenga msingi wake kutoka katika Maandiko Matakatifu
na Maadili. Yanaonesha haki na wajibu; mafao ya wengi na kwamba, sera za maendeleo
endelevu zinapaswa kumgusa mtu mzima: kiroho na kimwili kwani tatizo kubwa katika
ulimwengu wa utandawazi ni ukosefu wa usawa kati ya watu hali inayopelekea kinzani
na migogoro ya kijamii.
Usawa ni kikolezo kikubwa cha msingi wa maendeleo,
lakini kwa miaka mingi wachumi wengi wameliangalia jambo hili kwa jicho la makengeza.
Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kubainisha kwamba, utu na heshima ya binadamu
vinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika mipango ya maendeleo endelevu.
Kardinali
Turkson anaendelea kubainisha kwamba, Jamii nyingi zinakabiliana na changamoto za
utandawazi katika medani mbali mbali za maisha, changamoto inayojionesha kwa kasi
ya ajabu katika masuala: uharibifu wa mazingira; ongezeko kubwa na wahamiaji na watu
wasiokuwa na makazi maalum wanaotafuta maboresho na hifadhi ya maisha; kuna mwingiliano
mkubwa katika njia za mawasiliano ya jamii, kiasi kwamba, leo hii dunia imekuwa kama
Kijiji, bila kusahau kwamba, kuna kiasi kikubwa cha fedha na mtaji kinachovuka mipaka
ya nchi kama: mtaji, habari, kazi, mali ghafi na bidhaa.
Utandawazi unaopaswa
kuungwa mkono ni ule unaoshirikisha utajiri wa watu na tamaduni zao kuendelea kuchangia
katika ustawi na maendeleo ya ulimwengu mamboleo; huku uhuru, utu na heshima ya mwanadamu
vikipewa msukumo wa pekee. Binadamu kamwe anasema Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto
wa kumi na sita kuwa ni mdau wa utandawazi na wala si mwathirika wa utandawazi, anayetenda
kwa kuongozwa na mwanga wa akili timamu, upendo na ukweli. Mafao ya wengi na upendeleo
kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii ni jambo la kuzingatiwa kwa
kumwilisha mshikamano unaoongozwa na kanuni ya auni.
Kardinali Turkson anaendelea
kubainisha kwamba, utandawazi umekuwa ni chanzo cha kukua na kuenea kwa umaskini,
kinzani na migawanyiko. Hii inatokana na ukweli kwamba, hakuna mgwanyo sawa wa rasilimali
ya dunia. Kwa mfano utajiri na rasilimali inayopatikana Barani Afrika na kutoka katika
nchi zinazoendelea zimezitajirisha kwa kiasi kikubwa Nchi Tajiri duniani na Afrika
ikaendelea kutumbukia katika umaskini, magonjwa na njaa.
Ni Bara ambalo liliathirika
kwa kiasi kikubwa na biashara haramu ya utumwa, leo hii kuna utumwa mamboleo. Ili
utandawazi uweze kuwanufaisha watu wengi zaidi duniani, kuna haja ya kuhakikisha kwamba,
hata nchi changa zaidi duniani zinashiriki katika mchakato wa maoni, maamuzi na utekelezaji
wa mikakati inayowagusa. Huu ndio utandawazi unaowajibisha.
Utandawazi umekuwa
ni chanzo cha imani kwa wananchi wengi wanaoishi katika nchi changa duniani. Leo wengi
wao ni waamini wa dini na madhehebu mbali mbali hata kama kuna baadhi ya watu wameendelea
kubaki katika dini na imani zao za asili. Utandawazi umesaidia pia mwingiliano wa
shughuli za uchumi, biashara na masoko. Lakini, nchi hizi zinaendelea kunyonywa na
kuwafaidisha wachache ndani ya Jamii, ambayo wamejikuta wakiogelea katika kashfa za
rushwa na ufisadi wa mali ya umma. Makampuni makubwa ya kimataifa yamekuwa ni wakwepaji
wakubwa wa kodi ambayo ingeweza kusaidia mchakato wa maendeleo endelevu kwa nchi changa
duniani.
Kutokana na ukweli huu, anasema Kardinali Turkson kuna haja ya kuzingatia
kanuni maadili katika masuala ya utandawazi kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Mungu
na mwanadamu; kwa kuibua sera za uchumi zinazozingatia haki, utu na heshima ya mwanadamu;
kazi ipewe heshima yake na wafanyakazi wapate ujira unaokidhi mahitaji muhimu ya mwanadamu.
Mali itumike kwa ajili ya mafao ya wengi, kwa kuzingatia mshikamano unaosimamiwa
na kanuni ya auni, upendo na udugu bila kusahau kwamba, kuna haja ya kujipatanisha
na Mungu na jirani, ili kujenga na kuimarisha msingi wa utawala bora unaozingatia
sheria na kanuni za nchi.
Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa
la haki na amani anasema, athari za utandawazi mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa
zinaweza kuangaliwa katika misingi ya haki, mali, mshikamano, udugu, upatanisho, utawala
bora na kanuni ya auni. Maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili
wa Vatican iwe ni fursa ya kujichotea utajiri unaofumbatwa katika Nyaraka mbali mbali
za Mtaguso huo kwa maisha na utume wa Kanisa.
Baba Mtakatifu Francisko anawahamasisha
waamini na watu wote wenye mapenzi mema: kwanza kabisa kuwapenda na kuwathamini maskini;
kusimama kidete kulinda na kutetea amani sanjari na utunzaji bora wa mazingira. Jumuiya
ya Kimataifa inapaswa kushirikiana kwa dhati mintarafu mpango wa Mungu, aliyeumba
na kuona kwamba, kila kitu alichokuwa ameumba ni chema na kizuri.
Makala hii
imeandaliwa na Padre Richard Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.