Jitahidini kumfahamu Kristo ambaye ni mwamba amini, chemchemi ya furaha na uhuru wa
kweli!
Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Ibada ya Misa takatifu, Alhamisi tarehe
27 Juni 2013 kwenye Kikanisa cha Domus Sanctae Marthae kilichoko mjini Vatican amewakumbusha
waamini kukita imani yao katika mwamba thabiti ambao ni Yesu Kristo na kwamba, hakuna
Ukristo pasi na Kristo! Ni mwaliko kwa waamini kuonesha ile furaha ya maisha yao kwa
Kristo na Kanisa lake, kwani Kristo hapendi kuwaona watu "wenye nyuso zilizokunjamana
kama kigae na mioyo migumu kama jiwe"!
Wakristo wanapaswa kutolea ushuhuda
wa imani yao kwa njia ya matendo na kujipambanua kwa kusimama kidete kulinda na kutetea
ukweli. Wakristo wanaoonesha imani yao kwa njia ya matendo thabiti ni sawa na mjenzi
aliyejenga nyumba yake kwenye mwamba thabiti, kamwe haitaweza kutikisika. Mwamba huu
ni Neno la Mungu. Lakini, wale wanaopepeta mdomo katika maisha yao, watambue kwamba,
wanajenga nyumba katika mchanga na anguko lao ni kubwa!
Baba Mtakatifu anasema
kwamba, wale wanaomtegemea Kristo mwamba na ngome ya maisha yao, wataweza kuvuka magumu
ya maisha, hawa ndio Wakristo ambao wanamkumbatia na kumwamini Kristo na kamwe hawezi
kuwadanganya. Kuna Wakristo wanaojiita kuwa ni Wakristo lakini hawamwamini Kristo,
hawa ni wale wanaopotoka na kielelezo cha utepetevu wa imani katika ulimwengu mamboleo.
Kwa bahati mbaya anasema Baba Mtakatifu waamini kama hawa wamo hata ndani ya Kanisa.
Baba
Mtakatifu katika mahubiri yake amekazia kwa na namna ya pekee: umuhimu wa kumfahamu
Yesu Kristo ambaye ni mwamba amini, chemchemi ya uhuru wa kweli na watu wenye furaha
inayobubujika kutoka kwa Kristo, furaha ambayo wanawashirikisha wengine.
Ibada
hii ya Misa takatifu imehudhuriwa na viongozi na wafanyakazi kutoka katika idara ya
afya mjini Vatican.