2013-06-26 09:38:16

Watawa wanachangamotishwa kumhubiri Kristo kwa ari kubwa zaidi kama alivyofanya Mtakatifu Paulo, Mwalimu wa Mataifa!


Askofu Norman King'oo Wambua wa Jimbo Katoliki Bungoma, Kenya, hivi karibuni aliwaambia waamini kutoa kipaumbele cha kwanza katika kulinda na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kwani hapa ni mahali muafaka ambapo imani, utu na maadili mema yanarithishwa kwa namna ya pekee kutoka kwa wazazi kwenda kwa watoto wao. Wazazi wanaposhindwa kutekeleza dhamana na wajibu wao, hapo Kanisa linaweza kwenda mrama!

Askofu King'oo ameyasema hayo wakati wa Ibada ya Misa Takatifu wakati wa Nadhiri za daima kutoka kwa Masista wa Shirika la Mabinti wa Mtakatifu Paulo, kwenye Kanisa la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Kisoko, Mjini Busia. Katika Ibada hii, Sr. Janet Joan Angala, Sr. Praxides Walumbe na Sr. Metrine Nafula Waliama waliweka Nadhiri zao za daima.

Askofu King'oo amewashukuru na kuwapongeza wazazi kwa kuwalea na hatimaye, kukubali mabinti zao kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa kama watawa, wanaochangamotishwa kwa namna ya pekee, kufuata ari na mwamko wa utangazaji wa Habari Njema kama aliokuwa nao Mtume Paulo, Mwalimu wa Mataifa.

Ni mwaliko wa kufuata nyayo za Msimamizi wa Shirika lao, aliyebahatika kukutana na Yesu Mfufuka kwa njia ya ajabu, iliyomwezesha kutubu na kuongoka, akawa ni Mtangazaji hodari wa Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Yesu anapaswa kuwa ni dira na mwongozo kwa watawa katika hija ya maisha na utume wao kwa Kristo na Kanisa lake. Watawa wanapaswa kuboresha maisha yao kwa njia ya Sala, Tafakari ya Neno la Mungu pamoja na huduma makini kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Askofu King'oo amewakumbusha Mabinti wa Shirika la Mtakatifu Paulo kwamba, katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari, kuna kinzani na ukanimungu unaoenezwa kwa kasi ya ajabu na maendeleo haya, ni jukumu la dhamana yao kuhakikisha kwamba, wanalisaidia, tetea na kulilinda Kanisa kwa njia ya maisha na utume wao katika sekta ya mawasiliano ya Jamii. Anawataka watawa kujitoa kimasomaso bila ya kujibakiza, wanapojitahidi kuimwilisha nadhiri ya ufukara katika maisha yao.

Kukua na kukomaa kwa miito mbali mbali ndani ya Kanisa nchini Kenya ni mchango na dhamana inayofanyiwa kazi na Familia za Kikristo kwani wao ni uti wa mgongo wa maendeleo ya Kanisa katika kutekeleza kazi ya uumbaji na mwendelezo wa kazi ya ukombozi ambayo Kristo amelikabidhi Kanisa lake. Hata katika umasikini wao, Familia nyingi zimekuwa ni chemchemi ya miito mitakatifu ndani ya Kanisa.

Dhamana kwa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo ni Uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili, ni mwendelezo wa utume uliotekelezwa kwa ari kubwa na Mtakatifu Paulo, Mwalimu wa Mataifa.

Takwimu zinaonesha kwamba, katika Shirika la Mabinti wa Mtakatifu Paulo, kuna miito mingi inayoendelea kuibuka kutoka Barani Afrika, jambo ambalo wanamshukuru Mungu. Shirika hili lilianzishwa kunalo mwaka 1915 na Mwenyeheri James Alberione, Alba nchini Italia na linatekeleza utume wake katika nchi 52 duniani kote!







All the contents on this site are copyrighted ©.