2013-06-26 08:19:24

Shukrani kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania! Maaskofu wanaalikwa kuendelea kuwa ni sauti ya Kinabii kwa kusimamia Ukweli!


Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki Morogoro anapomshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumwezesha kusherehekea Jubilee ya Miaka 25 tangu alipowekwa wakfu kuwa Askofu wa Jimbo la Tanga na baadaye Jimbo Katoliki la Morogoro, anamshukuru Mwenyezi Mungu, Maaskofu na Watanzania katika ujumla wao. RealAudioMP3

Kwa namna ya pekee anapenda kuwashukuru Maaskofu wenzake, ambao wameonesha moyo wa upendo, umoja na mshikamano kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa na watanzania katika ujumla wao! Askofu Mkude ameyasema hayo wakati wa mahojiano maalum na Radio Vatican katika Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 25 tangu alipowekwa wakfu kama Askofu, sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, yaani hii ni zawadi mara mbili!

Matunda ya mshikamano na umoja huu ambao ni baraka na neema ya Mungu yanajionesha kwa namna ya pekee katika huduma zinazotolewa na Kanisa Katoliki katika sekta mbali mbali za maisha ya watanzania: katika afya, lakini zaidi katika elimu. Kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Mtakatifu Augustino cha Tanzania, SAUT, ilikuwa ni kati ya changamoto kubwa iliyofanyiwa kazi na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Leo hii SAUT imekuwa na kupanuka na ni kati ya Vyuo vikuu nchini Tanzania yenye wanafunzi wengi na iliyoeneza matawi yake sehemu mbali mbali za Tanzania.

Askofu Mkude anasema, si kwa bahati mbaya kwamba, Baraza la Maaskofu Katoliki liliamua kukipatia Chuo Kikuu cha Kikatoliki jina la Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa, kwani walitaka wanafunzi watakaobahatika kusoma katika Chuo hiki waweze kujitoa bila ya kujibakiza katika ujenzi wa "Mji wa Mungu"; wajitoe kwa ajili ya ustawi na maendeleo endelevu.

Hii ndiyo furaha ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania anasema Askofu Mkude na kwamba ni matunda ya mshikamano, umoja na sala, changamoto ya kusonga mbele kwa imani na matumaini thabiti.

Askofu Mkude anasema, Maaskofu wanapaswa kuendelea kuwa ni sauti ya kinabii nchini Tanzania kwa kusema na kutetea ukweli, hata ikiwa ni lazima watoe sadaka kubwa, kwani ukweli utawaweka huru! Ukweli huu usemwe katika medani mbali mbali ya maisha ya watanzania, kwani watu wanatarajia kusikia msimamo wa Kanisa katika masuala mbali mbali yanayogusa maisha yao.

Ni wajibu kwa Kanisa kuendelea kutoa mwanga utakaowawezesha waamini na wananchi kujipima mbele ya Mwenyezi Mungu na Jamii inayowazunguka; pale walipokosea, waweze kutubu na kufanya marekebisho! Pale walipofanikiwa, basi wamshukuru Mungu. Maaskofu wanayodhamana ya kuliombea Kanisa na Tanzania katika ujumla wake; wana dhamana ya kulielekeza Kanisa na Watanzania; kuwatia ari na moyo, kuwapa mwanga na faraja kwani Kanisa ni Mama wa wote.

Askofu Telesphor Mkude katika mahojiano maalum na Radio Vatican anaendelea kuiombea Tanzania: haki, amani, upendo, mshikamano, ustawi na maendeleo endelevu!







All the contents on this site are copyrighted ©.