Makleri wanachangamotishwa kuwa ni mababa wa neema na maisha ya kiroho katika utekelezaji
wa shughuli za kichungaji!
Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa
cha Domus Sanctae Marthae, kilichoko mjini Vatican, siku ya Jumatano asubuhi, tarehe
26 Juni 2013, amewachangamotisha waamini kuhakikisha kwamba, wanakuza ndani mwao ile
furaha ya kujisikia kwamba ni wazazi, jambo ambalo pia linapaswa kujionesha hata katika
maisha ya Makleri ambao kimsingi wanapaswa kuishi maisha ya useja. Kama hakuna furaha
ya kuwa baba, anasema Papa Francisko, hapo kuna kitu ambacho hakiendi sasa sawa!
Baba
Mtakatifu anasema, ubaba wa Makleri unajionesha katika utekelezaji wa mikakati na
majukumu ya shughuli za kichungaji. Hawa ni mababa wa maisha ya kiroho wanaoshiriki
dhamana ya kuwa ni mababa. Mababa wa familia wanalo jukumu la kuhakikisha kwamba,
wanalea, wanatunza na kuzihudumia familia zao, changamoto kwa waamini kuomba neema
ya kuwa kweli ni mababa wema na waaminifu wa familia.
Baba Mtakatifu anakiri
kwamba, kuna dhambi na mapungufu mengi yanayofanywa na mababa, lakini jambo moja kubwa
ni kwamba, wanaunganishwa na ile hamu ya kuwa ni mababa hata kama hawana watoto wao
wa kuzaa! Makleri wawe ni mababa wa neema na maisha ya kiroho katika shughuli za kichungaji
ndani ya Kanisa.
Kama Makleri, wanayo haki ya kumshukuru Mwenyezi Mungu anayewakirimia
zawadi ya kuwa ni mababa wa maisha ya kiroho ndani ya Kanisa. Abraham, Baba wa imani
ni kielelezo makini cha baba mwenye dhamana ya kulinda na kutetea familia. Mzee Simeoni
anaonesha ile liturujia ya furaha kwa kumwimbia Mwenyezi Mungu pale anapompokea Mtoto
Yesu alipopelekwa Hekaluni.