2013-06-26 14:56:22

Kanisa ni Hekalu la Roho Mtakatifu


Baba Mtakatifu Francisko katika katekesi yake kama sehemu ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani anaendelea kulichambua Kanisa kama Familia ya Mungu, mintarafu Kanuni ya Imani. Jumatano, tarehe 26 Juni 2013 ametafakari kuhusu Kanisa kama Hekalu la Roho Mtakatifu. Kristo alilinunua kwa damu yake azizi, akalijaza Roho wake na kulijalia misaada inayofaa kwa ajili ya umoja uonekanao na wa kijamii.

Baba Mtakatifu anasema, Hekalu la Selemani lililoko Mjini Yerusalem, mahali ambapo waamini walikutana na Bwana, lilikuwa ni kielelezo cha Kanisa. Yesu Kristo, Neno wa Mungu aliyetwaa mwili anaishi ndani mwa waamini wake, Yeye kimsingi ndiye Hekalu hai, mahali ambapo waamini wanaweza kukutana na Mwenyezi Mungu.

Kristo kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo anawapatia uwezo waamini kuwa ni mawe hai na sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Hapa ni mahali ambapo waamini kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo wanatekeleza dhamana ya ukuhani wao kwa kutolea sadaka takatifu ya maisha ya kiroho.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, Roho Mtakatifu kwa njia ya karama na mapaji mbali mbali anayowakirimia waamini, anawaunganisha na hivyo kuwawezesha pia kuchangia katika ujenzi wa utakatifu wa Kanisa. Katika utekelezaji wa dhamana hii kubwa anasema Baba Mtakatifu, kila mtu anapaswa kushiriki, kwa kutambua kwamba, ni jiwe hai na lenye thamani katika kupamba Hekalu la Mungu.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kusali ili kwamba, kila mmoja wao aweze kutekeleza wajibu wake katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kuongozwa na Roho Mtakatifu na kuwa, Yesu Kristo ndiye Jiwe kuu la Msingi. Baba Mtakatifu ametambua uwepo wa mahujaji wanaozungumza lugha ya Kiingereza, kati yao ni wale waliotoka Afrika ya Kusini.

Roho Mtakatifu awajaze moyo wa upendo na ari mpya, ili waweze kuishi kwa kufuata mfano wa Kristo. Anawakumbusha kwamba, mchoko na hali ya kukata tamaa itawafanya kushindwa kuwa kweli ni mawe hai na matokeo yake watajikuta wamejitenga na Kristo. Mwishoni, Baba Mtakatifu anasema ni matumaini yake kwamba, mkutano wa katekesi yake utawatia nguvu na ari ya kutangaza Habari Njema ya wokovu iliyoletwa na Yesu Kristo.







All the contents on this site are copyrighted ©.