Kardinali John Njue, Askofu mkuu wa Jimbo Kuu la Nairobi anaendelea kuwahimiza waamini
nchini Kenya na Afrika kwa ujumla kuhakikisha kwamba, wanajifunga kibwebwe kulitegemeza
Kanisa katika maisha na utume wake wa Uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu
mzima: kiroho na kimwili.
Kwa miaka mingi Wamissionari wamejitoa bila ya kujibakiza
kwa ajili ya kupandikiza mbegu ya imani ya Kikristo, wakaikuza na kuipalilia sasa
ni dhamana na jukumu la Waamini Barani Afrika kujitegemea na kulitegemeza Kanisa.
Kardinali Njue ameyasema hayo hivi karibuni alipokuwa anatabaruku Kanisa la
Parokia ya Mtakatifu Yosefu Mkasa, lililoko eneo la Kahawa Magharibi, Jijini Nairobi.
Amewashukuru na kuwapongeza waamini wa Parokia hii kwa kuonesha moyo wa ukarimu uliowawezesha
kujenga Kanisa kwa nguvu zao wenyewe bila ya kuhitaji msaada kutoka nje ya nchi. Parokia
hii itahudumiwa na Wamissionari wa Consolata.
Waamini wa Parokia ya Mukasa
wanaendelea kuhamasishwa kuhakikisha kwamba, wanakua na kuimarisha ari na wito wa
shughuli za Kimissionari, kwani hapa hakuna kulala hadi kieleweke! Watu wanasubiri
kusikia Habari Njema ya wokovu inatangazwa kwa ari kubwa zaidi kwa njia ya ushuhuda
wa maisha yao, kama kielelezo cha imani tendaji, hasa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha
Mwaka wa Imani.