Damu ya Azizi ya Kristo ni chemchemi ya Upatanisho
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita katika Waraka wake Africae
Munus, Dhamana ya Afrika anasema kwamba, haki, amani na upatanisho ni mawazo
makuu yaliyochaguliwa na Mababa wa Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu wa Afrika kwa
kutambua wajibu na dhamana ya Kanisa Barani Afrika katika wajibu wake wa kijamii na
kitaalimungu. Upatanisho na
haki ni misingi mikuu ya ujenzi wa amani. Amani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu
inayowajibisha binadamu. Amani bila haki ni kudanganyana na wala haiwezi kudumu kwa
muda mrefu. Haki ya binadamu inapaswa kuwa ni tunda la upatanisho katika ukweli unaoongozwa
na upendo. Haki ni fadhila fungamanishi katika maisha ya binadamu. Bila nguvu ya
upatanisho anaendelea kusema Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita kwamba,
mikakati na mchakato wa amani unakosa nguvu, mwelekeo na dira. Toba na wongofu wa
ndani ni jambo la msingi linaloweza kujenga na kuimarisha misingi ya haki na amani,
kwa kutambua nafasi na uwepo wa Mungu katika hija hii ya maisha ya mwanadamu. Upatanisho
unapata chimbuko lake katika upendo wa dhati, kama inavyojionesha katika maisha na
utume wa Yesu ambaye ni Mpatanishi kati ya Mungu na binadamu. Upatanisho unamwezesha
mwanadamu kujenga umoja na mshikamano wa kweli, changamoto kwa waamini kuwa kwelini
wajumbe wa upatanisho. Bara la Afrika kwa miaka mingi limejikuta likitumbukia
au kutumbukizwa katika kinzani, migogoro, vita na mafarakano, mambo ambayo yameacha
madonda ya kudumu katika maisha na mioyo ya watu, kumbe, upatanisho unapaswa kuwa
ni mchakato endelevu katika maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika. Upatanisho hushinda
matatizo, hurudisha heshima ya watu binafsi na hufungua njia ya maendeleo na amani
ya kudumu kati ya watu katika ngazi mbali mbali. Upatanisho linapaswa kuwa ni tendo
la kijasiri. Wahanga wana haki ya kujua ukweli na kupata haki. Ni katika mantiki
hii, Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Vikarieti ya Tanzania, kuanzia
tarehe 26 hadi tarehe 29 Juni 2013, kwenye Chuo Cha Mtakatifu Gaspar, Kola, Morogoro,
litakuwa na Semina kuhusu Damu ya Kristo chemchemi ya Upatanisho. Lengo ni kuendeleza
tafakari ya kina iliyotolewa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita,
itakayowawezesha waamini kuwa na maisha mapya katika Kristo, ambaye ndiye Mpatanishi
mkuu kati ya Mungu na binadamu. Damu ya Kristo ni mto wa rehema. Haya pia ni maandalizi
ya Maadhimisho ya Mwezi Julai, ambao kimsingi umetengwa na Mama Kanisa kwa ajili ya
Ibada kwa Damu Azizi ya Kristo; mwezi ambao unafunguliwa kwa Siku kuu ya Damu Azizi
ya Yesu inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe Mosi, Julai. Shirika la Wamissionari
wa Damu Azizi ya Yesu linajiandaa kuadhimisha Jubilee ya miaka 200 tangu lilipoanzishwa,
yaani tangu Mwaka 1815 hadi mwaka 2015. Upatanisho uwe ni mwanzo mpya katika Kristo
Mpatanishi.