Ulinzi na usalama kwa mahujaji ni jambo linalopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza wakati
wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani!
Kamati ya Maandalizi kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani kwa
mwaka 2013 huko Rio de Janeiro, Brazil, yanayotarajiwa kuanza kushika kasi hapo tarehe
22 hadi tarehe 28 Julai 2013 inasema, ulinzi na usalama wa mahujaji na wananchi katika
ujumla wao, unapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na vikosi vya ulinzi na usalama,
ili kuhakikisha kwamba, tukio hili la kihistoria linaadhimishwa katika mazingira ya:
Ibada, amani na utulivu.
Serikali ya Brazil imesema kwamba, vikosi vya ulinzi
na usalama vimekwisha jiandaa kwa ajili ya maadhimisho haya na kwamba, askari wamekwisha
kupangiwa maeneo ya ulinzi na usalama katika maeneo ambayo yatatumika kwa ajili ya:
Ibada, Katekesi na malazi. Wizara ya Mambo ya ndani ya nchi kwa kushirikiana na Wizara
ya Ulinzi na Usalama wamepewa dhamana ya kuhakikisha kwamba, ulinzi na usalama vinadumishwa
wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani inayoongozwa na kauli mbiu " Basi
enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa ni wanafunzi".
Dr. Domenico Giani, Kamanda
wa Vikosi vya Ulinzi na usalama vya Vatican anasema kwamba, wanaendelea kushirikiana
kwa karibu zaidi na Serikali ya Brazil ili kuhakikisha kwamba, Maadhimisho haya yanakwenda
kama yalivyopangwa. Katika siku za hivi karibuni wananchi wa Brazil wamekuwa wakifanya
maandamano kupinga ongezeko la gharama ya maisha kutokana na maandalizi ya Kombe la
Dunia litakalofanyika nchini humo kunako mwaka 2014, kwamba, hayana uhusiano wowote
na Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani.
Hili ni tukio la Kiimani linalosubiriwa
na wananchi wengi wa Brazil, anasema Askofu mkuu Joao Oran Tempesta, wa Jimbo kuu
la Rio de Janeiro, ambaye pia ni Rais wa Kamati ya Maandalizi kutoka Baraza la Maaskofu
Katoliki Brazil. Vijana wanaoandamana nchini Brazil wanataka kujenga utamaduni utakaowaletea
matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi; wanataka umoja, upendo na mshikamano wa
kweli. Kwa vijana Wakatoliki, Kristo anapaswa kuwa ni lengo lao kuu katika hija ya
maisha yao!
Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yanawashirikisha vijana wenye
fadhila za Kikristo, wanaotamani kuleta mabadiliko duniani kwa kuzingatia kwanza kabisa:
haki na amani; utu na heshima ya binadamu pamoja na mafao ya wengi. Askofu mkuu Joao
Oran Tempesta anasema, maandamano haya ni dalili kwamba, wananchi hawaridhiki na jinsi
ambavyo Serikali inavyoshughulikia masuala ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.
Wanasikitishwa
na kuenea kwa rushwa na ufisadi. Serikali ya Brazil inaendelea kufanya majadiliano
na waandamanaji hao ili kupata suluhu ya kudumu.