2013-06-25 15:11:00

Sinodi za Maaskofu ni matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican


Sekretarieti kuu ya Sinodi ya Maaskofu iliyoundwa kunako mwaka 2012 mara baada ya Maadhimisho ya Sinodi ya Uinjilishaji Mpya iliyojadili kuhusu Uinjilishaji Mpya kama nyenzo ya kutangaza Imani ya Kikristo, imehitimisha kikao chake cha nne, kilichofanyika hapa mjini Vatican, chini uongozi wa Askofu mkuu Nikola Eterovic.

Katika utangulizi, Askofu mkuu Eteovic amegusia kuhusu Maadhimisho ya Mwaka wa Imani ambao umeshuhudia matukio makubwa ya kihistoria: kwanza ni lile la Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwa hiyari na utashi kamili kuamua kung'atuka kutoka madarakani na badala yake, Papa Francisko kuchaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Wajumbe hao wamejadili kwa kina na mapana kuhusu Sinodi ya Maaskofu wa Kanisa Katoliki kutoka Mashariki na Sheria zao; Mabaraza ya Maaskofu Katoliki, Mabaraza ya Kipapa, Shirikisho la Wakuu wa Mashirika pamoja na taasisi ambazo zinashiriki kwa karibu zaidi katika Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu.

Wajumbe wa Sekretarieti pia walipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko, aliyewachangamotisha kuanza kutafakari kuhusu tema itakayofanyiwa kazi katika Maadhimisho ya Sinodi ya Kumi na nne ya Maaskofu. Alikumbusha kwamba, Sinodi za Maaskofu ni matunda ya Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, unaohimiza kwa namna ya pekee: umoja na mshikamano miongoni mwa Maaskofu.

Huduma hii nimuhimu sana kwa Kanisa katika Mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Sinodi zitaendelea kufanyiwa maboresho ili kukuza na kuimarisha mchakato wa majadiliano kati ya Maaskofu na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Sekretarieti ya Sinodi imepata nafasi ya kuweza kutafakari kwa kina tema, sababu na vigezo vilivyopelekea wajumbe hao kuweza kuchagua, ili hatimaye, Baba Mtakatifu aweze kutoa uamuzi wa mwisho. Wajumbe wa Sekretarieti ya Sinodi watakutana tena kuanzia tarehe 7 hadi 8 Oktoba, 2013







All the contents on this site are copyrighted ©.