SIGNIS yafuta Kongamano la Kimataifa huko Beirut kutokana na vita inayoendelea Syria
Kongamano la Kimataifa lililokuwa limeandaliwa na Shirikisho la Wanahabari Wakatoliki
Kimataifa, SIGNIS, ambalo lilitarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 20 hadi tarehe 23
Oktoba 2013 mjini Beirut, nchini Lebanon, limefutwa kutokana na machafuko ya kivita
yanayoendelea kupamba moto huko Syria.
Waandaaji wa kongamano hili pia nchini
Lebanon walionesha hali ya wasi wasi wa usalama wa wajumbe wa SIGNIS kutoka sehemu
mbali mbali za dunia. Mambo haya yote yamepelekea kufutwa kwa Kongamano hili, kama
alivyoeleza Bwana Augustine Loorthusamy, Rais wa SIGNIS.
Wamesikitishwa na
uamuzi huu, lakini SIGNIS inapenda kuonesha mshikamano wake wa dhati na wananchi wa
Syria wanaokabiliana na hali ngumu ya maisha kutokana na vita inayoendelea huko Mashariki
ya Kati. Wanasema, wanaendelea kuwasindikiza kwa njia ya sala na kwamba, Wakristo
huko Mashariki ya Kati wanao wajibu na dhamana ya kubaki na kuendeleza nchi yao, ingawa
maeneo mengi yameharibiwa kutokana na vita.
Huu ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa
kuhakikisha kwamba, inaendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini, upatanisho, haki
na amani; wananchi wanapaswa kuhamasishwa kutumia njia mbadala badala ya kukimbilia
mtutu wa bunduki kama suluhu ya kinzani na migogoro inayojitokeza huko Mashariki ya
Kati. Wananchi wamechoka na vita wanataka kuonja amani na matumaini mapya.
Licha
ya Kongamano hili la Kimataifa kufutwa, bado wajumbe wa SIGNIS watakutana katika mji
utakaopangwa baadaye. Hadi sasa Roma na Madrid ni kati ya miji inayopewa kipaumbele
cha kwanza.