Ukristo ni wito unaoonesha upendo wa Mungu kwa binadamu na kwamba, Yesu daima atawasaidia
wale wanaomkimbilia kwa imani na matumaini; hata katika shida na magumu, hakuna haja
ya kukata tamaa, bali kupiga moyo konde na kusonga mbele kwa ujasiri mkuu.
Ni
sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Maadhimisho
ya Ibada ya Misa Takatifu, Jumanne, tarehe 25 Juni 2013, kwenye Kikanisa cha Domus
Sanctae Marthae kilichoko mjini Vatican.
Baba Mtakatifu akifanya rejea kwenye
Liturujia ya Neno la Mungu anawaomba waamini na watu wenye mapenzi mema kuwa na busara
kama iliyooneshwa na Babu Abraham kwa kukumbatia amani pamoja na kujisalimisha mikononi
mwa Mwenyezi Mungu. Abraham ni kielelezo cha imani, matumaini na mapendo, hali ambayo
ilimwezesha kuwa ni Baba wa Mataifa.
Mwenyezi Mungu anaongea na kila mwamini
mmoja mmoja, kwani ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kila Mkristo ameitwa binafsi
na hakuna cha bahati mbaya, bali kila kitu ni sehemu ya mpango wa Mungu; ni wito unao
andamana na ahadi pamoja na wajibu! Baba Mtakatifu anasema, Yesu Kristo ni kielelezo
makini cha wito na wajibu huu kwani hata katika maisha yake alikumbana na vikwazo
na kinzani lakini hakukata tamaa kwani alimtegemea Mwenyezi Mungu katika kutekeleza
kazi ya ukombozi.
Waamini wanapaswa kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu ambaye
ni uhakika wa usalama wa maisha yao. Ukristo ni witona mwaliko wa upendo unaomwezesha
mwamini kuwa ni Mtoto mpendwa wa Mungu; ndugu yake Kristo. Ni wito ambao una raha,
magumu na changamoto zake. Jambo la msingi ni kila mwamini kuhakikisha kwamba, anakuwa
mwaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, kama alivyokuwa Abraham, Baba wa imani.
Waamini
wajitahidi kutunza ahadi za Ubatizo katika maisha yao. Pale wanapotumbukia katika
dhambi, wawe na ujasiri wa kusimama na kumwendea Yesu kwa moyo wa toba na majuto,
kwani amewaahidia wafuasi wake kwamba, atakuwa pamoja nao hadi utimilifu wa nyakati.
Ibada
ya Misa takatifu imehudhuriwa na viongozi waandamizi na wanafanyakazi kutoka Baraza
la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum, Taasisis ya Kipapa kuhusu
maisha pamoja na kituo cha unajimu cha Vatican.