Kardinali Leonardi Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya
Mashariki anaungana na viongozi wakuu na waamini wa Makanisa ya Mashariki kuomboleza
kifo cha Padre Francois Murad, aliyeuwawa kikatili siku ya Jumatatu, tarehe 24 Juni
2013 nchini Syria.
Marehemu Padre Murad amekumbukwa katika sala pamoja na
marehemu wote waliokwisha poteza maisha yao kutokana na vita inayoendelea nchini Syria
kwenye Kikanisa cha Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki.
Ukatili
wa namna hii hauwezi kukubalika, kuna haja kwa wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kusimama
kidete ili hatimaye, kuibua mbinu mkakati utakaosaidia kusitisha vita hii, ili hatimaye,
kuanza mchakato wa upatanisho, haki na amani. Ni matumaini ya Wakristo nchini Syria
kwamba, wataendelea kubaki na kushiriki katika utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu
kwa kuonesha ile sura ya Kristo.