2013-06-25 08:01:12

Kanisa nchini Pwani ya Pembe linajielekeza zaidi katika Uinjilishaji Mpya!


Baraza la Maaskofu Katoliki Pwani ya Pembe hivi karibuni limehitimisha mkutano wake wa kawaida wa tisini na sita uliochambua pamoja na mambo mengine: hali ya uchumi na fedha katika Kanisa na Taasisi zinazoendeshwa na kusimamiwa na Kanisa Katoliki nchini humo; mikakati na sera za maendeleo ya Kanisa, lakini zaidi changamoto ya Uinjilishaji Mpya; mkakati wa kichungaji unaopewa kipaumbele cha pekee na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. RealAudioMP3

Maaskofu wanamshukuru Mwenyezi Mungu kwa yale yote ambayo wamefanikiwa kuyatekeleza kama sehemu ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Kanisa limetoa mchango makini katika jitihada za kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho wa kitaifa, mara baada ya kutokea machafuko ya kisiasa nchini humo kunako mwaka 2010.

Padre Roberto Campisi, afisa kutoka Ubalozi wa Vatican nchini Pwani ya Pembe, amewachangamotisha Maaskofu Katoliki kuwekeza zaidi katika mchakato wa Uinjilishaji mpya, katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo, kwa kutoa fursa kubwa zaidi kwa waamini walei kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa, kwani wao wanatumwa ulimwenguni kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao adili.

Baraza la Maaskofu Katoliki Pwani ya Pembe, limeanzisha Tume ya Uinjilishaji Mpya, itakayobainisha sera na mikakati itakayotumiwa na Maaskofu katika utekelezaji wa dhamana ya Uinjilishaji nchini humo, kwa kuwaendea wale ambao kwa miaka ya hivi karibuni wamelegea na kuanza kusinzia katika imani.

Maaskofu wameamua pia kuanzisha Mfuko wa kulitegemeza Kanisa nchini humo kama sehemu ya changamoto iliyotolewa na Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu wa Afrika. Hili ni tatizo kubwa linaloendelea kukwamisha shughuli na mikakati ya maendeleo kwa Makanisa mengi Barani Afrika.

Maadhimisho ya Mkutano mkuu wa Mwaka wa Baraza la Maaskofu Katoliki Pwani ya Pembe, ilikuwa ni fursa pia ya kuweza kusikiliza kwa makini taarifa mbali mbali zilizotolewa na Wakuu wa Idara na Tume za Baraza la Maaskofu Katoliki; mafanikio, matatizo, fursa na changamoto zilizoko mbele yao. Mkutano mkuu wa 97 unatarajiwa kufanyika mwezi Januari 2014, kwenye Jimbo kuu la Gagnoa.








All the contents on this site are copyrighted ©.