2013-06-24 10:12:07

Serikali ina wajibu wa kusikiliza kilio cha raia wake! Lakini vurugu hapana!


Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil linasema, limekuwa likifuatilia kwa karibu zaidi matukio yanayoendelea kutokea nchini humo kuhusiana na kupanda kwa gharama za maisha na kuzorota kwa hali ya maisha kutokana na mchakato wa maandalizi ya Kombe la Dunia, litakalofanyika nchini Brazil hapo mwakani. Maaskofu wanapenda kuonesha mshikamano wao wa upendo na wananchi kwa wote wanaoshiriki katika maandamani ya amani kama njia ya kushirikisha mawazo na wasi wasi wao!

Kuna haja kwa wananchi wa Brazil kutambua tunu msingi na mipaka yake, ili kujenga Jamii inayosimikwa katika haki na udugu, hii ndiyo Jamii inapaswa kujengeka nchini Brazil. Maaskofu wanasema, maandamano haya miongoni mwa vijana yanachochewa kwa kiasi kikubwa na matumizi ya mitandao ya kijamii. Haya ni matokeo ya matatizo na changamoto ambazo hazikupewa ufumbuzi makini nchini Brazil.

Maandamano na vurugu zinazoendelea kwa sasa nchini Brazil ni matokeo na madhara ya rushwa na ufisadi uliokomaa ndani ya Jamii; ukosefu wa utawala wa sheria, kiasi kwamba, wananchi wanaamua kujichukulia sheria mikononi mwao! Ni matokeo ya ukosefu wa ukweli na uwazi, tunu msingi na kielelezo cha utawala bora. Pamoja na kuunga mkono wasi wasi wa wananchi kuhusu hatima ya maisha yao, Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil linasema, kamwe haliwezi kuunga mkono maandamano yenye vurugu na uvunjaji wa misingi ya haki na amani. Kanisa haliungi mkono matumizi ya nguvu dhidi ya vijana na waandamanaji.

Matatizo ya wananchi wa Brazil yanapaswa kushughulikiwa na wote, kila mtu akitekeleza wajibu na dhamana yake bila ya kutegea hata kidogo. Ni jukumu la kila raia kufuata sheria za nchi, mafao ya wengi, haki na amani na kwamba, kilio cha wananchi pia kinapaswa kusikilizwa na kamwe wasipuuzwe!








All the contents on this site are copyrighted ©.