2013-06-24 11:00:57

Jiaminisheni kwa Kristo na jitwikeni vyema Misalaba Yenu!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili asubuhi, tarehe 23 Juni 2013, aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa kushirikiana na Maaskofu wakuu 40 wanaoiwakilisha Vatican sehemu mbali mbali za dunia. Itakumbukwa kwamba, Mabalozi hawa wamekuwepo mjini Vatican kama sehemu ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake, alikazia umuhimu wa waamini kumfahamu Kristo kuwa ni Mwana wa Mungu aliye hai anayeendelea kufanya hija pamoja na wafuasi wake, wanaopaswa kujibu kutoka katika undani wa mioyo yao swali hili msingi ambalo Kristo anaendelea kuwauliza hata leo hii, wao wanasema kwamba, Yeye ni nani? Ni swali msingi katika hija ya maisha ya kiimani hata leo hii!

Ni changamoto na mwaliko wa kuonesha heshima na upendo mkuu kwa Kristo ambao umekuwa kweli ni nguzo na kielelezo cha maisha ya waamini. Jambo la msingi la kujiuliza ni ikiwa kama kweli waamini wenyewe wameyasimika mapendo yao kwa Kristo ambaye anapaswa kuwa ni kiongozi na mchungaji wao mkuu. Kamwe wasione aibu kumshuhudia mbele ya watu kama alivyofanya Mtakatifu Petro, licha ya mapungufu yake ya kibinadamu. Alimtumainia Kristo, akajiaminisha kwake, kiasi cha kumteua kuwa ni Mwamba ambao atajenga Kanisa lake juu yake.

Baba Mtakatifu amewaambia Maaskofu wakuu, wasisahau kuchukua vyema Misalaba ya maisha na utume wao na kumfuasa Kristo. Wakati mwingine Misalaba hii ni mizito, lakini waendelee kuthubutu kuomba neema kutoka kwa Kristo ili aweze kuwasaidia kuibeba Misalaba yao na kwa hakika hatawaacha pweke!







All the contents on this site are copyrighted ©.