Watoto kutoka katika familia za wakimbizi wanapaswa kulindwa, kuheshimiwa na kusaidiwa!
Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza linasema kwamba, Maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi
Duniani kwa Mwaka 2013 yamekuwa ni fursa nyingine kwa Jumuiya ya Kimataifa kuweza
kufahamu hali halisi inayoendelea katika maisha ya wahamiaji na watu wasiokuwa na
makazi wanaoteseka kutoka sehemu mbali mbali za dunia.
Baraza la Maaskofu Katoliki
Uingereza linaitaka Serikali ya Umoja wa Kitaifa kuhakikisha kwamba, inatoa kipaumbele
cha kwanza kwa: ulinzi, ustawi na maendeleo ya watoto inapokuwa ikishughulikia masuala
ya wahamiaji. Uingereza ni kati ya nchi ambazo zimetia sahihi kwenye itifaki ya kulinda
na kutetea haki msingi za watoto, kumbe, inapaswa kutekeleza jukumu hili kwa ufanisi
mkubwa.
Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza linaunga mkono taarifa ya pamoja
iliyotolewa na Tume ya haki msingi za binadamu kuhusu watoto waliotelekezwa na wazazi
wao nchini Uingereza. Taarifa hii inaonekana kwamba, inatoa kipaumbele cha kwanza
kwa masilahi kwa mtoto; kwa kuwalinda, kuwawezesha na kuwatetea.
Baraza la
Maaskofu Katoliki Uingereza linakumbusha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho
ya Siku ya wakimbizi Duniani kwa mwaka 2013, ameitaka Jumuiya ya Kimataifa kuonesha
moyo wa upendo na mshikamano kwa Familia za wakimbizi na wahamiaji, zinazoishi katika
mazingira magumu.
Hawa ni watu ambao wakati mwingine wanalazimika kuyakimbia
makazi yao, kiasi cha kukosa: amani, ulinzi na usalama. Ni familia ambazo zinakumbana
na nyanyaso ya kidini, kisiasa na kijamii. Ni familia ambazo wakati mwingine zinapokelewa
kwa macho ya makengeza kutokana na utofauti wa mambo mengi.
Baba Mtakatifu
Francisko anabainisha kwamba, kamwe waamini hawawezi kukaa kitako wakati ambapo ndugu
zao wanateseka kama wakimbizi. Familia hizi anasema Baba Mtaklatifu zinapaswa kupendwa,
kusaidiwa, kueleweka pamoja na kuonjeshwa ukatimu, kwani wao wanaonesha ile sura ya
Kristo Msulubiwa. Mwaliko huu ni muhimu sana kwa Kanisa na Jumuiya ya Kimataifa na
kwamba, wakimbizi wanayo nafasi ya pekee nchini Uingereza.