Vurugu na madhulumu ya kidini, si bure kuna mkono wa mtu kutoka Nje!
Kardinali John Onaiyekan, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Abuja, Nigeria, hivi karibuni
akishiriki katika mkutano wa majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na Waislam uliokuwa
umeandaliwa na Mfuko wa Kimataifa wa Oasis, Jimbo kuu la Milano, alisema kwamba, kinzani,
vurugu na mashambulizi yanayofanywa na baadhi ya waamini wa dini ya Kiislam wenye
misimamo mikali ya kidini nchini Nigeria, Syria na kwingineko ni mambo ambayo yanapandikizwa
kutoka nje.
Mfuko wa Kimataifa wa Oasis, hivi karibuni uliwakusanya viongozi
wakuu wa dini ya Kiislam na Kikristo ili kujadili kwa pamoja mbinu mkakati unaoweza
kufanyiwa kazi ili waamini wa dini hizi mbili waweze kuishi kwa amani, upendo na mshikamano
kama ilivyokuwa hapo awali, ambapo watu waliheshimiana na kuthaminiana hata katika
tofauti za dini na imani zao.
Lakini kwa miaka ya hivi karibuni mambo yamebadilika
sana, kinzani, migogoro na mauaji kwa kisingizio cha imani yameshika kasi kubwa sehemu
mbali mbali za dunia.
Wakristo na Waislam nchini Nigeria waliishi kwa amani
na utulivu, hadi miaka ya hivi karibuni hali ya hewa ilipochafuka baada ya kuibuka
kwa Kikundi cha Boko Haram ambacho tafsiri yake kwa lugha ya Kiswahili ingeweza kuwa
ni "Elimu ya nchi za Magharibi ni dhambi". Hiki ni Kikundi kinachopania kuhakikisha
kwamba, Nigeria inatawaliwa kwa "SHARIA" ya dini ya Kiislam. Kikundi hiki kilianzishwa
kunako mwaka 2002.
Tangu mwaka 2009 hadi sasa kuna zaidi ya watu 2,800 ambao
wamepoteza maisha yao kutokana na madhulumu ya kidini. Boko Haram mwanzoni hakikuwa
ni kikundi cha kigaidi, lakini pole pole kilianza kukataa kushirikiana na waamini
wa dini nyingine na hivyo kujitenga na matokeo yake, kikaanza kujiingiza katika madhulumu
ya kidini. Hiki ni kikundi ambacho kinapata misaada ya hali na mali kutoka nje ya
nchi.
Kuna baadhi ya raia kutoka nchi za nje wamekamatwa nchini Nigeria wakiwa
wanamiliki ghala kubwa ya silaha za kivita, huko Kano. Huu ndio mwelekeo wa vikundi
vya kigaidi kama Al Shabaab, kama kinavyojulikana Somalia; Al Qaeda, Mashariki ya
Kati; Taliban huko Pakistan. Ni Kikundi cha hatari kwani kinafanya mauaji kwa wote
bila kujali kitu.
Lakini ikumbukwe kwamba, si waamini wote wa dini ya Kiislam
wanaunga mkono Kikundi cha Boko Haram, Al Shabaab au Al Qaeda, kwani hawa wanachafua
dini na imani ya Kiislam kwa ajili ya masilahi yao binafsi, anasema Kardinali John
Onaiyekan. Kuna haja kwa waamini wa dini mbali mbali kusimama kidete kulinda na kutetea
utu na heshima ya binadamu; haki na amani pamoja na mafao ya wengi. Waamini washirikiane
kwa dhati katika mambo msingi na tofauti zao isiwe ni kisingizio cha kuanzisha fujo
na madhulumu bali utajiri unaopaswa kufanyiwa kazi kwa ajili ya mafao na ustawi wa
Jamii nzima.