Mtanzania ashika hatamu za kuliongoza Baraza la FAO..
Shirika la Chakula na Kilimo FAO, Ijumaa katika Kikao chake lilimchangua Balozi Wilfred
Joseph Ngirwa, kuwa Mwenyekiti mpya wa Baraza la FAO, kwa kipindi cha miaka miwili
ijayo June 2013 hadi June 2015.
Balozi Wilfred Ngirwa, amechaguliwa kushika
nafasi hii ya Mwenyekiti wa kujitegemea wa Baraza katika maana ya Mwenyekiti aliye
huru asiyegemea upande wowote, kwa shindi wa asilimia 96 kati ya kura zote zilizopigwa
na wajumbe wa Baraza 154, kura za ndio zikiwa 146, kura turufu 7 na kura za hapana
1( moja) .
Balozi Wilfred Ngirwa alizaliwa Tanzania mwaka 1948 katika familia
ya kawaida ya Watanzania,Bukoba Mkoani Kagera. Ni mtalaam katika uwanja wa Kilimo
na uchumi, kazi aliyoifanya wa muda wa miaka 38 , ambamo huduma yake ilitambulwia
vyema hasa kwa mchango wake kama Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Tanzania na katika
Mashirika matatu ya Umoja wa Mataifa yanayohusika na huduma kwa Mkulima, ambayo ni
Shirika la Chakula na Kilimo(FAO) Shirika la Mfuko wa Maendeleo katika Kilimo( IFAD),
na Shirika la Mpango wa Chakula (WFP). Na pia kama Mwakilishi wa Tanzania katika
mashirika hayo,uwakilishi uliompa heshima ya kuwa Balozi.
Katika Khafla ya
kumpongeza Balozi Ngirwa, iliyoandaliwa na Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini Italy,
Waziri wa Kilimo Tanzania, Mheshimiwa Waziri Christpher Kizza , alisema, ushindi
wa Balozi Ngirwa katika kinyanyang’iro cha cheo hicho, umekuwa ni ushindi na heshima
kubwa kwa Afrika, na hususani kwa Watanzania wote. Na hivyo ushindi huu ni changamoto
inayodai hasa tanzania kwa ujumla kuendelea kuishi kwa amani na utulivu, katika kudumisha
heshima ya Tanzania kwenye ngazi za Kimataifa, na kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania,
na hasa Wakulima na wafugaji vijijini.
Waziri aliomba ushirikiano wa karibu
na Mwenyekiti Mpya wa Baraza la FAO,akisema, ingawa kwa cheo chake hakifungamani na
upande wowote, bado Afrika inatazamia kunufaika zaidi na mchango wake, katika kubadili
maisha ya mkulima wa Afrika hasa kwa kutokana na uzoefu wake katika maisha yake ya
kawaida ya mkulima wa Afrika Vijijini.
Na Balozi James Nsekela , katika
hotuba yake fupi kwa Khafla hiii, alionyesha furaha yake kwamba Kupitia Balozi Ngirwa
, Tanzania imeaminiwa kuliongoza Shirika la FAO. Aliiaja kazi hii kuwa ni nzito na
nyeti yenye kuhitaji weledi na ushirikiano wa karibu na watendaji wengine. Vivyo katika
Khafla hii alikuwepo Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Zanzibar, Dr gharib .
Na
Balozi Ngirwa, alitoa shukurani zake za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Tanzania, Rais
Jakaya Kikwete, kwa kuidhinisha jina lake liwakilishwe FAO, kama mgombea wa cheo
cha Mwenyekiti wa kujitegemea katika Baraza la FAO. Na pia aliwashukuru wote, waliomtia
moyo wa kugombea kiti hicho. Na kwamba akiwa katika cheo hiki kipya atafanya kazi
zake katika misingi ya imani yake kwamba , FAO ni shirika ambamo misingi ya maamuzi
yake imesimikwa katika misingi ya makubaliano ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa.
Na hivyo, mamlaka yake yatazingatia rejea msingi zilizotajwa katika nyaraka za FAO,
na Mpango wa Kidharura wa Utendaji kama ilivyo ainishwa katika hati za makubaliano
za Fao.
Balozi Ngirwa anaanza Kazi yake Mpya Jumatatu 24 June 2013, katika
makao makuu ya FAO , Mjini Roma.
Alhamis iliyopita, Papa Fransisko alikutana
na wajumbe wa mkutano wa 38 wa FAO, ambamo katika hotuba yake Papa alikitaja kipeo
cha njaa duniani kuwa ni kashfa kwa nyakai hizi ambamo mataifa yanajiita kuendelea
na kustaraabika.
Na kwamba, kipeo hiki cha njaa dunaini hakiwezi kufutika
hadi hapo hali ya mazingira na maisha ya watu hasa vijijini , kuchunguzwa katika
mtazamo wa utu wa mtu na heshima yake kiutu.
Na alikumbusha kwamba, wote
wanajua moja ya jambo linalotendea vibaya maisha ya mamillioni ya watu duniani na
hasa vijijini ni ukosefu wa chakula, si tu kutokana na maafa asilia au migogoro
na vurugu za kisiasa zinazopokonya watu mlo wao wa kila siku, lakini pia ukosefu
wa uwajibikaji kwa walio nacho kutoa kwa wasiokuwa nacho ambao kwa wakati huu hutoa
kama mabaki kutoka meza ya chakula. Alisisitiza wanapaswa kuchota toka ghalani kile
kinachotakiwa kumfikia muhitaji mwingine kwa moyo wa upendo wa kweli..
Papa
ameonyesha imani yake kwamba , kwa uzoefu wa wajumbe wa Mkutano huo unaofanyika kwa
lengo la kushirikishana uzoefu na ufahamu utaweza kutoa mawazo ya kufaaa zaidi, kwa
ajili ya kusisimiua utendaji wa kimataifa kwa niaba watu maskini wahitaji vijijini
, wakiwa wamevuviwa si tu moyo wa hisani, ila upendo wa kweli katika kufuta kipeo
hiki cha njaa duniani.