Kanisa halina budi kujitegemea ili kutekeleza mikakati ya Uinjilishaji wa kina!
Kardinali John Njue, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Nairobi anasema, umefika wakati kwa
Kanisa nchini Kenya kujitegemea kama sehemu ya mchakato wa kuendeleza shughuli za
Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kardinali
Njue ameyasema hayo hivi karibuni wakati alipokuwa anazindua Jengo la Kituo cha Pacis,
lenye urefu wa ghorofa sita, litakalotumiwa na Kampuni ya Bima ya Pacis inayomilikiwa
na kuendeshwa na Kanisa Katoliki Kenya.
Kardinali Njue anasema kwamba, Kampuni
hii itakuwa ni kitega uchumi kikubwa kwa Kanisa Katoliki nchini Kenya, kitakachokuwa
na uwezo wa kusaidia kutoa ajira kwa vijana pamoja na maboresho katika sekta ya elimu,
afya, maendeleo na huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.
Kampuni ya Bima ya Pacis imeonesha kuanza kupata mafanikio makubwa na inaendeshwa
kisayansi na kimaadili katika kuwahudumia wateja wake.
Wazo la kuanzisha Kampuni
ya Bima lilianza kujitokeza kunako mwaka 1997 na kunako mwaka 2004 Kampuni hii ikasajiliwa
nchini Kenya na kuanza kufanya shughuli zake za biashara kunako mwaka 2005. Faida
inayopatikana imekuwa ni msaada mkubwa katika huduma kwa Kanisa na Jamii kwa ujumla.
Ni matumaini ya Kampuni ya Bima ya Pacis kwamba, wateja wake wataweza kuwa na amani
na utulivu baada ya kuwekeza katika Kampuni hii.