Hija ya watoto mjini vatican ili kukutana na kuzungumza na Papa Francisko!
Baraza la Kipapa la Utamaduni linaendelea kuwekeza tunu ya majadiliano katika maisha
ya watoto kwani linatambua kwamba, mtoto umleavyo ndivyo akuavyo! Hata katika utoto
wao wanalo jambo la kujifunza na kuwashirikisha wengine, ile furaha, imani na matumaini.
Ni kutokana na mwelekeo huu, Baraza la Kipapa la Utamaduni chini ya uongozi
wa Kardinali Gianfranco Ravasi, limeaanda tamasha maalum kwa ajili ya watoto kutoka
Jimbo kuu la Milano, watakaosafiri kwa Treni hadi mjini Roma siku ya Jumapili na kupokelewa
na Baba Mtakatifu Francisko. Kutoka Milano kutakuwa na jumla ya watoto 71 na watu
wazima 60; jumla yao wote ni watu 131.
Treni maalum kutoka Milano, itakapofika
mjini Bologna, watoto 115 watapanda, wakisindikizwa na watu wazima 50. Treni hii,
itakapowasili mjini Firenze, watoto 61 na watu wazima 40 watapanda ndani ya Treni
ili kuendelea na safari kuelekea kituo cha Treni cha Mtakatifu Petro, huko mjini Vatican
watapokelewa na Mwenyeji wao Baba Mtakatifu Francisko.
Jumla ya watu 397 watasafiri
na Treni maalum kutoka Milano hadi mjini Vatican ili kukutana na kuzungumza na Baba
Mtakatifu Francisko ambaye anaendelea kukazia umuhimu kwa jamii kuwalinda, kuwatunza
na kuwasaidia watoto kukua: kiroho, kimwili na kimaadili. Watoto watakuwa na mkutano
wao maalum kuanzia saa 7: 00 Mchana hadi Saa 9:30 Alasiri, watakapopanda tena Treni
na kurudi majumbani mwao.