Yaliyojiri G8 kwa Mwaka 2013: Biashara, Kodi na Uwazi
Mapambano dhidi ya ukosefu wa fursa za ajira kwa vijana ni kati ya vipaumbele vinavyofanyiwa
kazi na wakuu wa G8 mara baada ya kuhitimisha mkutano wake wa Mwaka uliohitimishwa
hivi karibuni huko Lough Erne, Ireland ya Kaskazini. Wakuu hawa wameahidi kubana matumizi
pamoja na kuendelea kutumia rasilimali na nyenzo zilizopo ili kuhakikisha kwamba,
wanatengeneza fursa za ajira kwa vijana.
Wachunguzi wa masuala ya kiuchumi
wanabainisha kwamba, hali ya uchumi kwa nchi wanachama wa G8 bado ni mbaya, ingawa
hali ya hatari imeondolewa kwa sasa. Sera ya fedha katika nchi wanachama inapaswa
kusaidia kuinua hali ya uchumi kwa kusimamia bei ya bidhaa na huduma ndani ya nchi
zao; kazi inayotekelezwa na Benki kuu.
Viongozi wa G8 wamekubaliana pia kimsingi
kwamba, watalivalia njuga tatizo la ukwepaji kodi na kwamba, wanaendelea kutekeleza
mikakati yao ya kiuchumi, kisiasa na kijamii kwa kuongozwa na "T,T,T" yaani, "Trade,
Tax and Transparancy" Yaani, Biashara, Kodi na Uwazi na kwamba, watashirikishana taarifa
ya mambo ya fedha na kwamba, wameanzisha vita kwa ngazi ya kimataifa dhidi ya "wajanja
wachache" wasiotaka kulipa kodi na wale wanaotumia fedha chafu kujijenga kiuchumi
na kisiasa.
Mchakato huu unapania kupata fedha ambazo zitatumika kwa ajili
ya kuwekeza kwenye medani mbali mbali za maendeleo kama mchakato unaopania kukuza
uchumi. Wakuu wa G8 wameelezea kwamba, wataendelea kufanya marekebisho katika mifumo
na miundo mbinu ili kufanya maboresho katika hali ya maisha ya raia wao; kuongeza
kasi ya ushindani, kutoa mikopo pamoja na kuwajengea uwezo wa mtaji wafanya biashara
wadogo wadogo.