Jubilee ni Kipindi cha furaha, shukrani, toba na msamaha!
Askofu Mkuu Josephat Louis Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha anamtakia kheri na baraka
Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki Morogoro, anapoadhimisha Jubilee ya Miaka
25 ya utume wa Kiaskofu. Kilele cha maadhimisho haya ni hapo tarehe 22 Juni 2013 kwenye
Seminari Ndogo ya Mtakatifu Petro, iliyoko Jimboni Morogoro.
Askofu mkuu
Lebulu anasema Jubilee ni kipindi cha furaha, shukrani, toba na msamaha. Askofu Mkude
ana kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya maisha lakini zaidi kwa
kumteua na kumweka wakfu kushiriki ukuhani wa Kristo katika: kufundisha, kuongoza
na kuwatakatifuza watu wa Mungu.
Ni kipindi cha toba na msamaha: kama binadamu
ana karama na mapungufu yake na wala hakuna sababu ya kuona aibu kumwendea Yesu na
kuomba msamaha ili kuonja tena upendo na huruma yake sanjari na kumpatia nafasi ya
kujazilia pale palipopungua kwa neema na baraka zake. Ukasisi ni dhamana kubwa ambayo
Kristo ameikabidhi kwa binadamu mwenye udhaifu, lakini Yeye mwenyewe anafahamu nini
cha kutenda.
Askofu Mkuu Lebulu anampongeza Askofu Mkude kwa mchango wake mkubwa
si tu katika kuwafundisha, kuwaongoza na kuwatakatifuza Watu wa Mungu Jimbo Katoliki
Tanga na Morogoro, lakini pia kwa miaka mingi amekuwa ni Mwenyekiti wa Idara ya Katekesi,
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Matunda ya kazi zake ni pamoja na Katekisimu
Mpya ya Kanisa Katoliki kwa lugha ya Kiswahili; Katekisimu ya Kanisa Katoliki, Ufupisho
Makini, vitabu ambavyo ni msaada mkubwa kwa maisha ya waamini na wote wenye mapenzi
mema wanaozungumza lugha ya Kiswahili.
Jubilee ya Miaka 25 ya Uaskofu ni kipindi
maalum kwa Askofu Mkude kumshukuru Mungu akiungana na Familia ya Mungu nchini Tanzania
kuendelea kuadhimisha Mwaka wa Imani sanjari na kumbukumbu ya miaka 20 tangu Mwenyeheri
Yohane Paulo wa Pili alipochapisha kwa mara ya kwanza Katekesimu Mpya ya Kanisa Katoliki,
muhtasari wa: Kanuni ya Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili yanayojikita katika
kumwilisha Amri za Mungu pamoja na Sala inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya
mwamini.
Askofu mkuu Josephat Lebulu anasema kwamba, kama Makasisi wao ni vyombo
mikononi mwa Mwenyezi Mungu anaweza kuwatumikia kadiri ya mpango wake katika maisha
na historia ya mwanadamu. Anamwombea Askofu Mkude ili aendelee kuwa ni chombo safi
na bora mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Awe ni daraja inayowaunganisha watu na Mungu
na Mungu na watu. Aendelee kuwaonjesha watu huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya
maisha na utume wake kama Askofu. Awe kweli ni kikolezo na chachu ya maendeleo endelevu,
daima akipania kuifanya dunia kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.