2013-06-21 09:15:45

Benki ya BADEA kugharimia miradi ya maendeleo nchini Tanzania


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, Alhamisi, Juni 20, 2013, amekutana na kufanya mazungumzo na wajumbe wa Bodi ya Benki ya Kiarabu kwa Maendeleo ya Afrika (BADEA) Ikulu, mjini Dar es Salaam. Katika mkutano huo, Rais Kikwete ameishukuru benki hiyo kwa kuendelea kuunga mkono jitihada za maendeleo ya Tanzania kwa misaada mbali mbali ambayo imekuwa inatolewa na Benki hiyo kwa Tanzania.

BADEA imekuwa inaunga mkono shughuli za maendeleo ya Tanzania tokea mwaka 1975 ilipofungua shughuli zake nchini na tokea wakati huo imetoa kiasi cha dola milioni 175 hasa katika maeneo ya elimu, miundombinu ya barabara na maji.

Katika mazungumzo hayo, ujumbe huo wa BADEA ukiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Benki hiyo, Bwana Abdelaziz Khelef umemweleza Rais Kikwete uamuzi wa Benki hiyo kusaidia mradi wa maji wa Mwanga-Same katika Mkoa wa Kilimanjaro na pia kuangalia uwezekano wa kusaidia miradi ya kusambaza umeme vijijini.

Wiki hii, Serikali ya Tanzania ilitiliana saini mkataba na Benki hiyo ambako BADEA itagharimia mradi wa kusambaza maji katika maeneo ya Mugango, Kiabakari na Butiama Mkoani Mara, ujenzi wa Barabara ya Wete-Chakechake, Kisiwani Pemba na kutoa msaada wa kiufundi kwa Kituo cha Hesabu cha Pan African kilichoko Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Aidha, Rais kikwete amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa kampuni ya kimataifa ya Marekani, General Electric ukiongozwa na Bwana John Rice, Makamu Mwenyekiti wa kampuni hiyo katika mazungumzo yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam. Katika mazungumzo hayo, kampuni hiyo imemweleza Rais Kikwete kuhusu dhamira yake ya kuwekeza katika uchumi wa Tanzania kwa nia ya kuunga mkono mwono wa Maendeleo ya 2025.








All the contents on this site are copyrighted ©.